Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amemuagiza mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara ya Bigwa–Kisaki (km 78) kuhakikisha anafanya matengenezo ya mara kwa mara katika maeneo yanayotumiwa na wananchi wakati ujenzi ukiendelea, ili kuondoa adha ya usafiri na kupunguza gharama za usafirishaji.
Ulega ametoa agizo hilo, mkoani Morogoro, alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo. Pia ametoa maelekezo ya moja kwa moja kwa TANROADS na mkandarasi kuhakikisha barabara hiyo inapitika wakati wote, hata ujenzi ukiwa unaendelea.
Amesema haikubaliki kwa wananchi kuendelea kutumia barabara yenye mashimo makubwa wakati mkandarasi yupo eneo la mradi, akisisitiza kuwa matengenezo ya mara kwa mara ni sehemu ya wajibu wake.
"Ni lazima barabara ipitike vizuri katika eneo lote ambalo ujenzi unaendelea. Hili si jambo la hiari, bali ni wajibu wa mkandarasi kuhakikisha wananchi hawapati usumbufu," amesema Ulega.
Ameongeza kuwa hakuna sababu ya kuiacha barabara ikiwa na mashimo mengi kiasi cha kushindwa kupitika, akisisitiza kuwa matengenezo ya kawaida lazima yafanyike wakati wote ili wananchi waendelee kupata huduma bora za usafiri.
Aidha, Waziri Ulega amemuelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro kuhakikisha anamrejesha mkandarasi katika barabara ya Kinole–Madamu (km 10) haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kufanya matengenezo ya dharura na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Shaban Taletale, amemueleza Waziri Ulega kuwa wananchi wana imani na Serikali katika kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ili waweze kupata huduma bora za usafiri na kufikiwa na maendeleo yaliyokusudiwa.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Patrick Rambika, amesema ujenzi wa barabara ya Bigwa–Kisaki ulianza mwezi Septemba 2025 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2027.
Amefafanua kuwa mradi huo unatekelezwa na mkandarasi China Railway 15 Bureau Group Corporation chini ya usimamizi wa TECU.






No comments:
Post a Comment