![]() |
| Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, akizungumza na wadau wa sekta ya madini wilayani humo akiagiza utekelezaji wa hatua za haraka za kudhibiti utoroshaji wa dhahabu. |
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amekutana na wadau wa sekta ya madini wilayani humo na kuagiza utekelezaji wa hatua za haraka za kudhibiti utoroshaji wa dhahabu, akisisitiza kuwa kila mdau anapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa shughuli za madini ili kulinda rasilimali za taifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Nkinda amesema mapambano dhidi ya utoroshaji wa madini ni ya kudumu na yanahitaji ushirikiano wa serikali, wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wote wa sekta hiyo huku akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kukiuka sheria.
Miongoni mwa maelekezo aliyoyatoa ni kuhakikisha dhahabu yote inayozalishwa inauzwa kupitia Soko la Madini la Kahama au vituo rasmi vya ununuzi vilivyosajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Pia ameelekeza kuwa dhahabu inayosafirishwa nje ya Mkoa wa Kimadini Kahama lazima ipate kibali kutoka Ofisi ya Madini kabla ya kusafirishwa.
Aidha, ameagiza maeneo ya mialo ya madini yasiwe ndani ya makazi ya wananchi na kuwataka wamiliki wa mialo waliobadilisha maeneo ya shughuli zao kutoa taarifa kwa Ofisi ya Madini kwa ajili ya mwongozo, Vilevile amesisitiza kuwa ni marufuku kuuza dhahabu kwa wanunuzi wasio rasmi maarufu kama makota, akieleza kuwa hatua hizo zinalenga kuongeza uwazi katika biashara ya madini na kulinda mapato ya Serikali.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Kahama, Chone Malembo, amesema serikali imeongeza ufuatiliaji baada ya matukio mawili ya kukamatwa kwa watuhumiwa waliokuwa wakisafirisha dhahabu nje ya utaratibu, huku taarifa zikionyesha walikuwa wametoka Kahama.
Malembo amesema kufuatia matukio hayo, kamati ya usalama ilifanya operesheni katika maeneo ya migodi ambapo ilibaini changamoto mbalimbali ikiwemo kuchanganyika kwa shughuli za uchimbaji na makazi ya wananchi, kutokuwepo kwa taarifa sahihi za uzalishaji katika baadhi ya mialo pamoja na uwepo wa wanunuzi wa dhahabu wasio rasmi.
Amesema baada ya operesheni hiyo na utoaji wa elimu kwa wadau, kiasi cha dhahabu kilichopelekwa kwenye Soko la Madini la Kahama kiliongezeka, hali ambayo inaonyesha kuwa baadhi ya dhahabu iliyokuwa haipelekwi kwenye mfumo rasmi sasa imeanza kuuzwa kupitia soko linalotambuliwa na serikali.
Katika kikao hicho, Meneja wa Mgodi wa Kandi, Mdaki Shaban, amesema kampuni yake imetekeleza maelekezo ya serikali kwa kutenganisha shughuli za uchimbaji na makazi ya wananchi, hatua iliyosaidia kuongeza usalama katika eneo la mgodi na kuboresha mazingira ya kazi.
Naye Baraka Emanuel mdau wa madini ameihauri serikali kuendelea kuboresha mazingira ya biashara ya madini kwa kupitia upya baadhi ya makato na gharama zinazowakabili wachimbaji, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kupunguza vishawishi vya utoroshaji wa madini na kuongeza mauzo kupitia masoko rasmi.
Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za serikali za kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania kwa mujibu wa sheria.




No comments:
Post a Comment