![]() |
| Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akiwasili katika hafla ya kufunga Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). |
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Arusha) |
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), ameielekeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuendelea kusimamia kwa umakini, uadilifu na weledi utekelezaji wa majukumu yake ya msingi kwa kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana katika michakato yote ya ununuzi wa umma.
Mhe. Munde alitoa maelekezo hayo wakati akifunga Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma mwaka 2026 lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
“PPRA mnatakiwa kuendelea kuimarisha usimamizi wa mfumo wa ununuzi wa umma kwa kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinazingatiwa kikamilifu, sambamba na kusukuma mbele matumizi ya teknolojia ya kidijitali ili kuongeza uwazi, uwajibikaji, ushindani na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma”, alisema Mhe. Munde.
Mhe. Munde alisema kuwa, taasisi zote nunuzi zinatakiwa kuendelea kutumia Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST) katika hatua zote za ununuzi kuanzia usajili wa wazabuni, uchakataji wa zabuni, usimamizi wa mikataba hadi malipo, kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410.
Vilevile, alizitaka taasisi nunuzi kuzingatia kikamilifu masharti ya kisheria yanayotoa upendeleo kwa wazabuni wazawa na kampuni za ndani, ikiwemo kuhakikisha zabuni zote zenye thamani isiyozidi shilingi bilioni 50 zinatolewa kwa kampuni za wazawa.
Mhe. Munde alisema kuwa, taasisi hizo zinapaswa kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi wa mwaka kwa ajili ya zabuni zinazolenga makundi maalumu ya kijamii, yakiwemo ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu, huku zikihakikisha makundi hayo yanajengewa uwezo na kulipwa kwa wakati.
Aidha, Mhandisi Munde alisisitiza umuhimu wa kutekeleza ununuzi endelevu kwa kuzingatia gharama za bidhaa katika mzunguko wake wote wa matumizi, matumizi bora ya rasilimali, hifadhi ya mazingira pamoja na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Munde aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya PPRA, taasisi zinazosimamia ununuzi wa umma, wadhamini, wawezeshaji, watoa mada, Maafisa Ununuzi na Ugavi, wadau wengine kwa mchango wao uliofanikisha kongamano hilo.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuimarisha mfumo wa ununuzi wa umma na ugavi ili uwe na ufanisi, uwazi, ushindani na ushirikishwaji, kwa lengo la kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa tija na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba, aliahidi kuwa Mamlaka hiyo itaendelea kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Naibu Waziri Munde kwa kuhakikisha Mamlaka hiyo inakuwa chachu ya maendeleo ya nchi.
Aidha, aliwataka washiriki wa Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma, kurejea katika taasisi zao wakiwa mabalozi wa mageuzi ya ununuzi wa umma na kuhakikisha maarifa na maazimio waliyoyapata yanatekelezwa kwa vitendo ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.








No comments:
Post a Comment