Uwekezaji unaofanywa na Serikali katika miradi ya maji ili kuhudumia wananchi umetoa matokeo kwa kuimarisha huduma ya maji katika jiji la Dodoma ambapo upatikanaji maji umeimarika kutoka asilimia 64.7 hadi asilimia 81.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema hayo akiwasilisha taarifa ya Upatikanaji maji na Usambazaji maji katika jiji la Dodoma kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, katika kikao Bungeni Dodoma.
Amesema jumla ya pampu za kusukuma maji 101 zinafanya kazi ya kufikisha huduma kwa wakazi wa Dodoma
Mhe. Aweso ameainisha Wizara ya Maji imepokea maelekezo yote ya Kamati na kujipanga kuwa bora zaidi katika huduma kwa jamii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga (Mb), pamoja na mengine ameelekeza kazi zaidi ifanyike kupunguza upotevu wa maji (NRW) ambao umetoka asilimia 40 hadi asilimia 33 ili wateja zaidi wapate huduma ya maji kwa kuongeza mtandao wa huduma ya maji.
Mhe. Kiswaga amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali kufikisha huduma ya maji katika jamii na kusisitiza pamoja na miradi ya majisafi inayoendelea, teknolojia itumike katika usafi wa mazingira ili maji machafu yanayotibiwa yaweze kutumika katika shughuli za jamii ikiwamo kilimo na ujenzi.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) inahudumia wananchi, ikiwemo Bahi, Kongwa, Chamwino na Dodoma mjini.












No comments:
Post a Comment