Na Mwandishi Wetu - Arusha
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara zinazoingia uwanja wa AFCON pamoja na maegesho ya magari huku ukiahidi kuhakikisha uwanja huo unafikika kwa barabara ya lami ndani ya muda uliokusudiwa.
Meneja wa TARURA mkoa wa Arusha, Mhandisi Nicholas Francis amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa takribani kilomita 13 za barabara za lami zitakazorahisisha usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo na wageni watakaohudhuria mashindano ya AFCON 2027.
Amefafanua kuwa mradi unajumuisha ujenzi wa barabara ya Essuri yenye urefu wa kilomita 2.45 kwa njia nne, barabara ya Lendita yenye kilomita 2.75 kwa njia nne, barabara ya Mateves AFCON–Bondeni City yenye kilomita 5.5 kwa njia moja na kilomita 2.1 kwa njia nne pamoja na barabara za mzunguko zenye urefu wa kilomita 1.5 zinazojengwa kwa njia nne.
Mhandisi Francis amesema mradi ulianza rasmi tarehe 20 Aprili, 2026 na unatarajiwa kukamilika 20 Mei, 2027 ukiwa na muda wa utekelezaji wa miezi 13.
"Kwa sasa ujenzi umeelekezwa katika ujenzi wa barabara ya Mateves AFCON–Bondeni City pamoja na barabara za mzunguko ili kuhakikisha ifikapo mwisho wa mwezi Oktoba mwaka huu uwanja mpya wa michezo ufikike”amesema
Ameeleza kuwa utekelezaji wa barabara ya Mateves AFCON–Bondeni City umefikia asilimia 53 huku mkandarasi akifanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati. Aidha, katika eneo la daraja la barabara ya Essuri, kazi zinaendelea kwa saa 24 kila siku.
"Tunatarajia ifikapo mwisho wa mwezi Agosti mwaka huu utekelezaji wa Barabara ya Mateves utafikia asilimia 85 endapo hakutakuwa na changamoto kubwa hususan mvua", amesema.
Amesema baada ya fidia kulipwa kwa watu waliopitiwa na mradi huo, kasi ya utekelezaji imeongezeka kwa kiwango kikubwa. Tuna imani kwamba ifikapo mwezi Desemba mwaka huu ujenzi wa barabara ya Mateves AFCON–Bondeni City utakuwa umekamilika kwa asilimia 100", amesema.
Kukamilika kwa mradi huo hakutasaidia tu kufanikisha maandalizi ya AFCON 2027 bali pia kutaimarisha mtandao wa barabara jijini Arusha, kupunguza msongamano wa magari, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuacha urithi wa miundombinu bora itakayowanufaisha wananchi kwa vizazi vijavyo.





No comments:
Post a Comment