Na Mwandishi Wetu
WAMIKI wa vituo vya kulelea watoto nchini wamehimizwa kuwekeza katika mafunzo ya kitaalamu kwa walezi ili kuboresha ubora wa huduma za malezi na makuzi ya awali ya watoto, kufuatia kuongezeka kwa mahitaji ya wataalamu katika sekta hiyo.
Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Future World Institute Robert Mkolla wakati wa mkutano wa wadau wa Umoja wa Vituo vya Kulea Watoto Tanzania (UVIKUWA), uliondaliwa na Ofisa Ustawi wa Jamii Kanda ya Saba Chanika wilayani Ilala chini ya uratibu wa Future World Institute baada ya kufunguliwa kwa tawi jipya la chuo hicho katika eneo la Chanika kwa Ndevu.
Mkolla amesema mafunzo hayo yameandaliwa kujibu ongezeko la mahitaji ya walezi wenye taaluma, linalochochewa na kuongezeka kwa vituo vya kulelea watoto kutokana na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi pamoja na ongezeko la wazazi wanaojihusisha na shughuli za uzalishaji mali.
Amesema programu hiyo inaendana na Sera ya Elimu ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023, inayomtaka kila mtoto kupata elimu ya awali kabla ya kuanza darasa la kwanza, hatua iliyoongeza mahitaji ya huduma bora za malezi na makuzi ya awali.
Kwa mujibu wa chuo hicho, mafunzo hayo yatawawezesha walezi kupata maarifa na stadi za kitaalamu kuhusu ukuaji wa mtoto, afya, usalama na elimu ya awali, hivyo kuboresha huduma zinazotolewa katika vituo vya kulelea watoto.
Aidha, amesema programu hiyo ya mafunzo itachangia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana, hususan wahitimu wa kidato cha nne, kwa kuwapatia ujuzi unaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri katika sekta ya malezi ya watoto.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Vituo vya Kulea Watoto Tanzania (UVIKUWA), Shabani Kibabi, amesema mafunzo hayo yataimarisha viwango vya malezi katika vituo vya kulelea watoto na kuchangia ustawi wa watoto kwa kuwawezesha walezi kupata ujuzi na taaluma stahiki.
Amesema kupitia mkutano huo washiriki wamejengewa uwezo katika ujasiriamali na mbinu za kuongeza kipato, hatua itakayowasaidia kuboresha uendeshaji wa vituo vyao sambamba na utoaji wa huduma bora za malezi.
Awali Mwenyekiti wa UVIKUWA Mkoa wa Dar es Salaam, Muhina Mwarabu, amewahimiza walezi na wamiliki wa vituo vya kulelea watoto kutumia fursa hiyo ya mafunzo, akisema ada ya Shilingi 800,000 ni nafuu na itawawezesha watu wengi zaidi kupata taaluma ya malezi ya watoto, hatua itakayoinua ubora wa huduma za malezi nchini.









No comments:
Post a Comment