MKUTANO WA KIMATAIFA WA AFYA YA MSINGI KUWAKUTANISHA WADAU ZAIDI YA 2,500 ARUSHA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, August 1, 2026

MKUTANO WA KIMATAIFA WA AFYA YA MSINGI KUWAKUTANISHA WADAU ZAIDI YA 2,500 ARUSHA




Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 


Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi unatarajiwa kuwa jukwaa la kuibua suluhisho na mikakati mipya ya kuboresha huduma za afya duniani, huku ukiwakutanisha zaidi ya washiriki 2,500 kutoka mataifa mbalimbali katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) kuanzia Septemba 9 hadi 11, mwaka huu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume, amesema mkutano huo utailetea Tanzania fursa ya kuonesha mafanikio yake katika utoaji wa huduma za afya ya msingi pamoja na kujifunza uzoefu kutoka mataifa mengine.

Amesema washiriki wa mkutano huo watatoka katika sekta mbalimbali zikiwemo taasisi za afya, vyuo vikuu, taasisi za utafiti, washirika wa maendeleo, watunga sera na wabunifu wa teknolojia za afya kutoka ndani na nje ya nchi.

"Kwa mara ya pili tunaandaa mkutano huu kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa huduma za afya ya msingi, ambazo ndizo msingi wa mifumo imara ya afya na maendeleo ya taifa. Pia tunataka kuonesha hatua kubwa ambazo Tanzania imezipiga katika sekta hii na kujifunza kutoka kwa mataifa mengine," amesema Dkt. Mfaume.

Amesema mkutano huo utatoa nafasi kwa wataalamu kuwasilisha matokeo ya tafiti zao, kubadilishana uzoefu na kujadili sera na teknolojia mpya zitakazosaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Dkt. Mfaume, Tanzania imeendelea kuimarisha huduma za afya ya msingi kwa kuongeza upatikanaji wa huduma kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya hadi hospitali, hatua ambayo imeifanya kuwa miongoni mwa nchi zinazotambuliwa kwa mafanikio katika eneo hilo.

Naye Dkt. Pius Kagoma amesema afya ni agenda ya kimataifa inayohitaji ushirikiano wa mataifa, hivyo mkutano huo utatoa fursa kwa washiriki kujifunza kutokana na uzoefu wa Tanzania na nchi nyingine katika kuimarisha huduma za afya ya msingi.

"Afya ya taifa moja ina mchango katika afya ya dunia. Tunataka mataifa mengine yaone hatua ambayo Tanzania imefikia na yajifunze, huku nasi tukijifunza kutoka kwao ili kuendelea kuboresha huduma zetu," amesema.

Ameongeza kuwa maandalizi ya mkutano yanaendelea vizuri, huku waandaaji wakishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha wageni watakaoshiriki wanapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini.

Amesema hatua hiyo inalenga kutumia mkutano huo sio tu kama jukwaa la majadiliano ya kisekta, bali pia kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii wa mikutano, uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa.

Mkutano huo unatarajiwa kuwaleta pamoja viongozi wa sekta ya afya, wataalamu, watafiti, wabunifu wa teknolojia, watunga sera na washirika wa maendeleo kutoka sehemu mbalimbali duniani, ukiwa na lengo la kuharakisha utekelezaji wa huduma bora za afya ya msingi kwa manufaa ya jamii.


No comments:

Post a Comment