UTEKELEZAJI WA DIRA 2050 UNAHITAJI MAAMUZI MAGUMU - KUSILUKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 30, 2026

UTEKELEZAJI WA DIRA 2050 UNAHITAJI MAAMUZI MAGUMU - KUSILUKA


Na Mwandishi Wetu - Arusha 


Serikali imezitaka Bodi na Menejimenti za mashirika ya umma kufanya maamuzi magumu na ya haraka katika kutekeleza majukumu yao, lakini ikisisitiza kuwa kasi hiyo lazima izingatie misingi imara ya sheria, uwajibikaji na utawala bora.

Akifunga Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum 2026) jijini Arusha jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Mpogole Kusiluka, alisema miaka ya mwanzo ya utekelezaji wa Dira 2050 ni muhimu kwa sababu maamuzi yanayofanywa sasa yataathiri kwa kiasi kikubwa kasi na ubora wa maendeleo ya nchi katika miaka ijayo.

“Kikao Kazi hiki kinafanyika katika wakati muhimu sana katika historia ya Taifa letu. Dira 2050 si jambo la siku zijazo tena. Utekelezaji wake umeanza,” alisema.

Alisema maamuzi yanayofanywa sasa, uwekezaji unaoanzishwa, taasisi zinazojengwa na viongozi wanaoandaliwa vitaamua kwa kiasi kikubwa safari ya Tanzania kuelekea mwaka 2050.

Balozi Kusiluka alisisitiza kuwa kufanikisha Dira hiyo kunahitaji viongozi kuwa tayari kufanya maamuzi yenye uzito na kuchukua hatua kwa wakati, akionya dhidi ya maazimio yasiyokwenda sambamba na mabadiliko yanayohitajika.

“Tusije na maazimio mepesi mepesi,” alisema.
Hata hivyo, alisema wito wa kuongeza kasi ya maamuzi haupaswi kutafsiriwa kama kuachana na taratibu na misingi inayosimamia utendaji wa Serikali.

Alisema kasi ya utekelezaji inapaswa kwenda sambamba na utawala bora, uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria, huku taasisi zikitumia mifumo ya Serikali kupata ufafanuzi wa masuala ya kisheria ili maamuzi yafanyike kwa wakati na kwa usahihi.

“Tunataka taasisi zetu ziwe na ujasiri wa kufanya maamuzi na kusonga mbele, lakini zifanye hivyo ndani ya misingi imara ya sheria, uwajibikaji na utawala bora,” alisema.

Katika maelekezo yake kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Balozi Kusiluka alisema taasisi za umma zinapaswa kupimwa kwa viashiria vikubwa vya utendaji vinavyoonyesha matokeo halisi, badala ya kujilinganisha na taasisi ambazo zenyewe hazifanyi vizuri.

“Benchmark yetu isiwe taasisi nyingine ambazo hazifanyi vizuri. Tulinganishe na wenzetu mahali kwingine duniani wanaofanya vizuri zaidi,” alisema.

Akizungumzia nafasi ya vijana, alisema Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi iko tayari kutoa kibali cha kuajiri vijana katika nafasi za uongozi, hususani katika vitengo vya ubunifu, hata kama hawana uzoefu mrefu, ikiwa wana sifa adimu na za kipekee zinazoweza kuongeza tija katika taasisi na Taifa.

Alisema pia sekta ya umma na binafsi zinapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano na kwamba ana imani taasisi zote zitaoanisha mipango yao na Dira 2050.

Akizungumzia hoja za ukaguzi, Balozi Kusiluka alisema maelekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hayapaswi kuchukuliwa kama jambo la kukamilisha kwa ajili ya ukaguzi pekee, bali yatumike kuimarisha mifumo, kudhibiti vihatarishi na kuzuia hoja zinazojirudia.

Alisema mashirika ya umma yana nafasi ya pekee katika utekelezaji wa Dira 2050 kutokana na mchango wao katika uzalishaji, biashara, usafirishaji, nishati, uwekezaji na huduma.

Balozi Kusiluka pia alisisitiza umuhimu wa taasisi kufanya kazi kwa pamoja na kutekeleza maazimio ya C-CEOs Forum, akisema hayapaswi kuwa hitimisho la mkutano bali mwanzo wa kazi.

Alisema tayari amefahamishwa kuhusu utekelezaji wa maazimio yote tisa ya mkutano wa mwaka jana na amefurahishwa kuona hatua nzuri imefikiwa katika maeneo mengi.

“Kwa hiyo, msiyachukulie maazimio haya kama hitimisho la Kikao Kazi; yachukulieni kama mwanzo wa kazi,” alisema.

Alizitaka taasisi kuhakikisha kila kiongozi anaelewa jambo linalomhusu, kinachopaswa kubadilika na matokeo yanayopaswa kuonekana, huku maazimio yakiwekwa katika mipango ya utekelezaji ya kila taasisi kadri itakavyofaa.

Balozi Kusiluka alisema utekelezaji wa Dira 2050 pia utategemea amani, usalama, utulivu na taasisi imara.

“Mazingira haya ndiyo yanayowezesha uwekezaji kufanyika, biashara kukua, wananchi kufanya kazi kwa utulivu na Taifa kupanga mustakabali wake kwa kujiamini,” alisema.

Alisema kipimo halisi cha mafanikio ya C-CEOs Forum kitaonekana baada ya washiriki kuondoka Arusha, kupitia ubora wa maamuzi, kasi ya utekelezaji, utatuzi wa changamoto, ushirikiano, thamani inayoongezwa katika rasilimali na matokeo kwa wananchi.

“Msiache mawazo mazuri yabaki katika ukumbi huu. Msiache mahusiano mliyojenga yaishie Arusha. Na zaidi ya yote, msiruhusu maazimio mliyokubaliana yawe kumbukumbu nzuri ya Kikao Kazi; yafanyeni yawe sehemu ya matokeo ya taasisi zenu,” alisema.

Akizungumzia juhudi za kuimarisha utendaji wa taasisi za umma, Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa, aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa mageuzi inayoyafanya, lakini akisema bado kuna kazi kubwa mbele kutokana na matarajio makubwa ya wananchi.

“Nina imani kwa weledi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, tutafika tunakotaka kufika,” alisema.

Akizungumzia mwelekeo huo, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema mashirika ya umma yanapaswa kuhamisha mtazamo kutoka kupima mafanikio kwa shughuli zinazotekelezwa kwenda katika kupima matokeo na thamani inayozalishwa kwa Taifa.

Alisema hilo linahitaji tija, ufanisi, ubunifu na matumizi ya teknolojia, huku rasilimali za Serikali zikitumika kwa uangalifu na uwekezaji ukitoa thamani inayopimika.
Kwa mashirika ya kibiashara, Bw. Mchechu alisema utendaji unapaswa kuonekana katika tija, uendelevu na faida, huku taasisi zinazotoa huduma za umma zikizingatia ubora, upatikanaji na ufanisi wa huduma.

C-CEOs Forum 2026, unaoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, ulifanyika Arusha kuanzia Septemba 28 hadi 30, ukiwakutanisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi na mashirika ya umma 320 pamoja na wadau wengine chini ya kaulimbiu “Mashirika ya Umma yenye Ufanisi wa Juu, kwa Uchumi Shindani, Shirikishi na Imara katika Kutekeleza Dira 2050."

No comments:

Post a Comment