WAKULIMA NA WAFUGAJI WAMECHANGIA UHIMILIVU WA UCHUMI, USALAMA WA CHAKULA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 30, 2026

WAKULIMA NA WAFUGAJI WAMECHANGIA UHIMILIVU WA UCHUMI, USALAMA WA CHAKULA



Na Shua Ndereka, OKULY BLOG, Morogoro


Wakulima na Wafugaji nchini wamechangia kuleta uhimilivu wa uchumi na usalama wa chakula kutokana na uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo kutosheleza mahitaji ya nchi hatua ambayo imetajwa kulifanya taifa kuwa na utulivu wakati huu ambao kuna vita kubwa za kiuchumi duniani.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa wakati wa kufungua Kongamano la Kitaifa la Wakulima Wadogo na Mkutano Mkuu wa 31 wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima (MVIWATA) linalofanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba hadi Oktoba Mosi, 2026 Mkoani Morogoro.

Balozi Dkt. Bashiru amesema nchi inajivunia kuwa na wakulima na wafugaji wanaozalisha chakula cha kutosha, ambao wamekuwa nguzo muhimu katika kuimarisha usalama wa chakula na kueleza umuhimu wa kujadili changamoto zinazowakabili wakulima wadogo, ikiwemo uhakika wa ardhi, kilimo ikolojia na masoko ya mazao, katika jitihada za kuelekea uhuru wa chakula.

Aidha, ametumia jukwaa hilo kutoa onyo kwa wakulima na wafugaji kuacha kujichukulia sheria mkononi na kusababisha uhasama unaoweleta madhara baina yao ikiwemo kujeruhiana na vifo.

Pia ameitaka MVIWATA kutafuta taarifa sahihi kwa kushirikiana na mamlaka ya Hali ya hewa, kuhusu tahadhari na namna ya kukabiliana na Mvua za El Nino, hatua itakayopunguza upotoshaji unaowapa hofu wakulima na wafugaji.

Katika hatua nyingine, ameupongeza mtandao wa MVIWATA kwa kutimiza miaka 33 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 na kuendelea kufanya mikutano yake mikuu kila mwaka tangu kusajiliwa rasmi mwaka 1995.

Kuhusu uwepo wa Agenda ya uchaguzi kupitia mkutano mkuu wa MVIWATA, Balozi Dkt. Bashiru amewataka wanachama wa Mtandao wa Vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) kutoruhusu siasa za mgawanyiko katika mchakato wa uchaguzi na kuwakumbusha kuchagua viongozi wanaowafaa kuelekea katika uchaguzi wa Viongozi wa mtandao huo Oktoba mosi mwaka huu.

‎"Tumieni Katiba yenu kuwachagua viongozi na si kuokota okota barabarani na kulinda taasisi kwa wivu mkubwa, kwa kufanya hivyo mtaepuka siasa za mgawanyiko ambazo zinaweza kunyoofisha MVIWATA na uchumi wa nchi" amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) Bw. Apollo Chamwela ameomba serikali kwa kushirikiana na wadau kuangalia namna ya kuwakopesha ng'ombe wa maziwa wakulima wadogo ili waweze kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na usalama wa chakula kwa ujumla.

"Kundi hili la wakulima wakipewa Mifugo katika maeneo ambayo mradi huu unatekelezwa, kwani itachangia mzunguko wa uzalishaji katika mbolea itakayopelekwa shambani na tutazalisha chakula salama" amesema Chamwela.

Akijibu Ombi la Mwenyekiti wa MVIWATA, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema serikali kwa kushirikiana na Benki, Viwanda vya maziwa zinazotekeleza mradi wa Kopa Ng'ombe Lipa Maziwa ili kukaa na kujadili namna ya kupanua wigo wa ukopeshaji wa ng'ombe wa maziwa ili kuongeza uzalishaji katika mazao yatokanayo na ufugaji wa Ng'ombe.

Baadhi ya Wakulima ambao ni Wanachama wa MVIWATA wametoa maoni na kero zao zinazohitaji utatuzi wa haraka, ambapo Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameahidi kuzipeleka serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi.


No comments:

Post a Comment