CGP KATUNGU ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA GEREZA JIPYA LA MFANO MSALATO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 22, 2026

CGP KATUNGU ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA GEREZA JIPYA LA MFANO MSALATO


Ssgt Mawazo Mtondo na Wdrs Irine Nkana - DODOMA.


Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, leo Oktoba 22, 2026, amewapongeza Askari mafundi wanaoshiriki ujenzi wa Uzio wa Gereza Jipya la Mfano Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya katika utekelezaji wa mradi huo uliopo Msalato Jijini Dodoma.

CGP Katungu ametoa pongezi hizo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa uzio wa gereza hilo, wenye urefu wa mita 950, ambao umefikia wastani wa asilimia 45 ya utekelezaji. Katika ziara hiyo, alikagua uzio huo kwa kuuzunguka ndani na nje ili kujionea maendeleo ya kazi.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, CGP Katungu amesema amekuwa akifuatilia maendeleo ya ujenzi huo mara kwa mara, kwa kufanya ziara binafsi au kuwatuma wasaidizi wake. Aidha, amewapongeza mafundi kwa kujituma, kufanya kazi kwa moyo na kwakuzingatia viwango vinavyokubalika.
“Niwapongeze mafundi wote kwa kazi nzuri na kubwa ambayo mmekuwa mkiifanya. Mmeifanya kazi hii kwa moyo. Kwa kweli, nimekuwa nikija kukagua mara kwa mara, ama kuja mwenyewe au kuwatuma wasaidizi wangu. Kazi ni nzuri sana,” amesema CGP Katungu.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Mhandisi wa Miradi, Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Ambrose Sostenes, amesema kazi zinazoendelea ni pamoja na kusuka boksi za nguzo mlalo za kati, kuandaa nondo za nguzo na ringi, kufunga boksi, kumwaga zege kwenye nguzo wima na mlalo, kujenga vidungu vya ulinzi katika kona za kuta za gereza, pamoja na kumwagilia maji kwenye sehemu zilizojengwa.

Aidha, ASP Sostenes amesema CGP Katungu amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa katika kufanikisha ujenzi huo kwa kuhakikisha mahitaji yote muhimu ya mradi yanapatikana kwa wakati.

No comments:

Post a Comment