SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA URATIBU NA UPATIKANAJI WA MAFUNZO TARAJALI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 22, 2026

SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA URATIBU NA UPATIKANAJI WA MAFUNZO TARAJALI


Na, Mwandishi Wetu – Dar es Salaam


Serikali inaendelea kuweka mkazo maalum kwenye kuboresha mfumo wa uratibu na upatikanaji wa mafunzo ya utarajali (internship) kwa kuwapatia wahitimu wa kada mbalimbali, uzoefu na ujuzi unaohitajika kwa lengo la kuwafanya wahitimu hao kuwa shindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Akiongoza kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam Oktoba 22, 2026, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Jim Yonazi, amesema maboresho yanayoendelea kufanyika ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, aliyoyatoa wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma (C-COEs Forum 2026) tarehe 28 Septemba, 2026 jijini Arusha.

Katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma, Mhe. Makamu wa Rais alielekeza kuandaliwa kwa mpango wa mafunzo kwa vitendo utakaowawezesha angalau vijana 10,000 kupata uzoefu katika mashirika ya umma na wengine 20,000 kwenye sekta binafsi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususani nguzo ya pili inayosisitiza maendeleo ya watu na rasilimali watu nchini.

Katika kikao hicho cha Makatibu Wakuu, Dkt. Yonazi amesema kuwa Serikali inaendelea kuweka kipaumbele kikubwa kwenye masuala ya mafunzo kwa vitendo (internship) kwa wahitimu ili kuziba pengo la kutokuwa na uzoefu, na kuwapa wahitimu hao uwezo wa kuunganisha elimu ya darasani na uhalisia wa mazingira ya kazi pamoja na kuongeza ushindani kwenye soko la ajira.

“Mafunzo ya ujuzi na uzoefu wa kazi yanapatikana kupitia taasisi mbalimbali za Serikali, vyuo vya ufundi, na programu za kitaifa zinazolenga kuwaandaa vijana kuwa shindani katika soko la ajira”, ameeleza Dkt. Yonazi.

Kikao hicho kiliwashirikisha Makatibu Wakuu wa kisekta kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Ujenzi.

No comments:

Post a Comment