DKT. MWIGULU AONGOZA MJADALA KUHUSU UWEKEZAJI KWENYE KILIMO BIASHARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 21, 2026

DKT. MWIGULU AONGOZA MJADALA KUHUSU UWEKEZAJI KWENYE KILIMO BIASHARA


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji kwenye kilimo na akawataka wenye mitaji waje kuwekeza Tanzania ambapo wataweza kufikia soko la watu milioni 170 kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Uwekezaji unaweza kuchangia kutoa huduma za chakula na lishe na wakati huohuo ukatengeneza fursa za kiuchumi zinazoonekana. Kwa hiyo, tunawakaribisha nyote kuwekeza nchini Tanzania kwani mnapowekeza Tanzania, kwa maana pana, mnawekeza pia katika soko la ukanda mzima,” alisema.
 
Akieleza fursa zilizopo, alitaja usindikaji na ufungashaji wa mazao, maghala, miundombinu ya kuhifadhi bidhaa katika ubaridi, usafirishaji, huduma za kidijitali na huduma za kifedha kwa wakulima na wafanyabiashara.
 
Ameyasema hayo jana (Jumanne, Oktoba 20, 2026) wakati akiongoza mjadala kuhusu uwekezaji kwenye kilimo biashara uliowahusisha viongozi wa kampuni za utafiti wa kilimo na teknolojia za kilimo, uzalishaji bidhaa za kilimo, mbegu na dawa za wadudu wa mazao yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue), jijini Des Moines, Jimbo la Iowa, Marekani.
 
Akifafanua, Dkt. Mwigulu alisema Tanzania ina hekta milioni 44 za ardhi inayofaa kwa kilimo, lakini zinazotumika ni hekta milioni 10.8 pekee. Kuhusu kilimo cha umwagiliaji, alisema nchi ina uwezo wa kumwagilia hekta milioni 29.4, lakini kwa sasa zinazotumika ni hekta 727,28 hali inayotoa fursa kubwa kwa wawekezaji.
 
Dkt. Mwigulu alisema Serikali imewekeza katika skimu za umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu na programu za kuwawezesha vijana kushiriki katika kilimo, mifugo na uvuvi. Vilevile, imeweka vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kwa wawekezaji.
 
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa sekta binafsi ni mshirika muhimu katika kuongeza thamani ya mazao, kupanua masoko, kutengeneza ajira zenye staha na kuimarisha usalama wa chakula na lishe.
 
Akichangia mjadala huo kuhusu matumizi ya Akili Unde (AI) katika kilimo, Mkurugenzi Mtendaji wa Utafiti na Viwanda wa Kampuni ya Microsoft, Dkt. Ranveer Chandra alisema alianzisha programu ya kilimo ndani ya Microsoft miaka 10 iliyopita na tangu wakati huo, wametekeleza shughuli mbalimbali nchini Tanzania.
 
“Miongoni mwa shughuli hizo ni ushirikiano wetu na MADE Alliance, ambao ulilenga kusaidia matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali kwa wakulima 50,000 wa alizeti nchini Tanzania. Pia tulishirikiana na kampuni ya Mawingu kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na intaneti katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.”
 
Kuhusu kuongeza ujuzi wa akili unde, Dkt. Ranveer Chandra alisema wameshirikiana na ABSA Tanzania pamoja na Women in Tech kutekeleza mpango unaolenga kuwapatia wanawake 5,000 mafunzo kuhusu akili unde.
 
“Akili unde inaweza kusaidia kuongeza kipato cha wakulima, kuboresha tija ya uzalishaji na kupunguza upotevu wa mazao. Ndani ya Microsoft, tumekuwa tukichunguza namna akili unde inavyoweza kutumika kufanikisha malengo hayo. Tunashirikiana na nchi mbalimbali, maeneo tofauti na taasisi nyingi katika kuendeleza teknolojia hii,” alisema.
 
Alisema akili unde haipaswi kuchukuliwa kama mbadala wa mkulima, bali kama nyenzo ya kuongeza maarifa na uwezo wa mkulima kufanya maamuzi sahihi. “Wakulima hufanya maamuzi mengi kila siku. Kwa mfano, baadhi ya maamuzi kuhusu wakati wa kupanda, kuvuna na kumwagilia mazao hufanywa kwa kukisia au uzoefu binafsi, bila kuwa na taarifa zote zinazohitajika.”
 
“Kupitia akili unde, tunaweza kupunguza utegemezi wa makisio na kuwawezesha wakulima kufanya maamuzi yanayotegemea taarifa sahihi zaidi. Changamoto moja muhimu tunayojaribu kutatua ni namna ya kufanya teknolojia hii iwe nafuu na iweze kufikiwa na wakulima wengi,” alisema.
 
Alisema Tanzania ina faida zaidi kutokana na nafasi yake ya kimkakati kama lango la kuunganisha masoko ya kikanda. “Tanzania inaweza kuwa mfano wa kituo cha kikanda cha akili unde kwa ajili ya kilimo, ambacho nchi nyingine katika ukanda huu zinaweza kujifunza kutoka kwake. Tunapozungumzia kituo cha kikanda cha akili unde kwa ajili ya kilimo, hatumaanishi tu mfumo unaoweza kujibu maswali bali tunahitaji mifumo inayoweza kutoa majibu sahihi na yanayofaa kwa mazingira ya Tanzania.”
 
Naye, Mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya CeluNova kutoka Mexico, Bw. Adolfo Vidal Ruiz alisema wanazalisha nyuzi kutoka kwenye majani ya nanasi na kuzitumia kama malighafi mpya katika utengenezaji wa karatasi za chooni na taulo za karatasi za jikoni (kitchen paper towels).
 
“Tayari tumefanikiwa kutengeneza karatasi za chooni kwa kutumia nyuzi za nanasi. Karatasi hizi zina uwezo mkubwa wa kufyonza maji na ni imara zaidi, yaani zinastahimili kuvutwa na haichaniki haraka ikilinganishwa na karatasi nyingine za chooni.”

No comments:

Post a Comment