DKT. MWIGULU AZUNGUMZA NA WAWEKEZAJI, WANADIPLOMASIA CHATHAM HOUSE, LONDON - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 10, 2026

DKT. MWIGULU AZUNGUMZA NA WAWEKEZAJI, WANADIPLOMASIA CHATHAM HOUSE, LONDON


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amekutana na wawekezaji na wawakilishi mbalimbali katika taasisi ya utafiti na uchambuzi wa masuala ya kimataifa Chatham House, jijini London, Uingereza na kuwaelezea vipaumbele vya kitaifa kwa sasa.

Chatham House ni kituo cha utafiti na ushauri wa kimkakati ambacho kazi yake kuu ni kuwaleta pamoja wataalamu, wasomi na watafiti ambao hufanya utafiti wa kina kuhusu masuala magumu ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiteknolojia, au usalama.

Mazungumzo hayo yaliwajumuisha wawakilishi wa taasisi za fedha za kimataifa, benki za biashara, mashirika ya kimataifa, wanadiplomasia, taasisi za utafiti na mashirika ya sera za maendeleo na wawakilishi wa Serikali.

Dkt. Mwigulu ambaye yuko Uingereza kwa ziara ya kikazi ya siku tano, alitumia jukwaa hilo kuwafikishia salamu za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwathibitishia dhamira ya Serikali ya kuimarisha ushirikiano na Uingereza pamoja na washirika wa kimataifa na wawekezaji.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu alielezea matarajio ya Tanzania chini ya DIRA 2050 na akafafanua vipaumbele vya mabadiliko ya kiuchumi vya Serikali na kuwashirikisha wadau hao wa kimataifa juu ya uwekezaji, ufadhili wa miundombinu, ushirikiano wa kikanda na ushirikiano wa kimataifa.

Dkt. Mwigulu aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kwamba Tanzania imeamua kubadilisha muundo wa uchumi wake kwa kuondoka katika utegemezi wa mauzo ya nje ya nchi ya bidhaa ghafi za kilimo na madini na kujielekeza kwenye usindikaji, utengenezaji na uongezaji wa thamani ndani ya nchi.

Alisisitiza kuwa ukuaji wa uchumi lazima uwe jumuishi, kuzalisha ajira na kuhakikisha kuwa faida za maendeleo zinawafikia idadi kubwa ya watu. “Tanzania imehama kutoka kwenye upangaji wa mipango na sasa iko kwenye utekelezaji wa DIRA 2050 ambapo inatafuta wabia wenye uwezo wa kutoa matokeo ya kiuchumi yanayoonekana,” alisema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu alikutana pia na wawakilishi wa Benki ya Standard na kusisitiza umuhimu wa kuelekeza ufadhili kwenye uwekezaji wenye tija kwa lengo la kupanua ushiriki wa sekta binafsi. Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa wananchi.

Mwakilishi wa Benki ya Standard anayesimamia masuala ya Afrika alimthibitishia Waziri Mkuu kwamba Tanzania inabakia kuwa moja ya masoko yake ya kipaumbele ya uwekezaji barani Afrika. Aliipongeza Serikali kwa uwekezaji wake mkubwa katika miundombinu na matumizi mazuri ya ufadhili uliopatikana kupitia mipango ya awali.

Alisema kuwa maendeleo ya miundombinu ya Tanzania na matarajio ya kiuchumi yameimarisha imani ya wawekezaji wa kimataifa na kuongeza ushindani kati ya taasisi za fedha za kimataifa zinazotaka kufadhili miradi nchini.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu alikutana na wawakilishi wa taasisi ya Private Infrastructure Development Group (PIDG) ambayo ni taasisi ya maendeleo ya uwekezaji wa miundombinu, maendeleo ya miradi, dhamana na fedha. PIDG inaungwa mkono na serikali sita za Uingereza, Sweden, Uholanzi, Uswisi, Australia na Canada. Uingereza, kupitia Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO), imekuwa mshirika mkuu wa ufadhili tangu kuanzishwa kwa PIDG takriban miaka 25 iliyopita.

Katika majadiliano yao, walieleza nia yao kupanua uwekezaji wa PIDG nchini Tanzania, kuimarisha ushirikiano wa umma na sekta binafsi (PPPs), kufadhili miundombinu ya kimkakati, na kutambua fursa za ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za miundombinu.

Kupitia GuarantCo, miaka mitano iliyopita PIDG ilitoa dhamana ya dola milioni 50 kwa Benki ya CRDB na kutokana na utekelezaji wake mzuri, mwaka 2025 dhamana iliongezwa na kufikia dola milioni 100.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu aliwapongeza PIDG kwa mchango wake katika sekta ya fedha ya Tanzania, maendeleo ya miundombinu na ukuaji wa sekta binafsi. Alisema kuwa utaalamu wa kiufundi wa PIDG unalingana na maeneo ya kipaumbele ya Tanzania, hasa miundombinu, mawasiliano ya simu, bandari, nishati na uwezeshaji wa uwekezaji.

Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ, Dkt. Juma Malik Akil, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitilla Mkumbo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angella Kairuki, Makatibu Wakuu na Watendaji Wakuu wa TISEZA na ZIPA.

No comments:

Post a Comment