Na Mwandishi Wetu - Mzuzu, Malawi.
Uongozi wa Hospitali ya Mzuzu nchini Malawi umeishukuru timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa Mzuzu, kwani hatua hiyo imeleta matumaini mapya kwa wagonjwa waliokuwa wakihitaji matibabu ya kitaalamu.
Makamu Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Mzuzu, Dkt. Wiseman Phiri, amesema katika siku tano ambazo timu ya BMH imetoa huduma hospitali hiyo, imefanikiwa kuwahudumia wagonjwa ambao awali walikuwa wamekata tamaa ya kupata matibabu ya kibingwa kutokana na changamoto mbalimbali za upatikanaji wa huduma hizo. Amesema ujio wa madaktari hao umeongeza fursa kwa wananchi kupata huduma stahiki karibu na maeneo yao.
Dkt. Phiri ameongeza kuwa uwepo wa timu hiyo haujaishia katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa pekee, bali pia umechochea hamasa ya kubadilishana maarifa na kuongeza ujuzi miongoni mwa madaktari wa Hospitali ya Mzuzu. Aidha, amesema ushirikiano huo umeimarisha zaidi uhusiano wa kitaalamu kati ya Hospitali ya Mzuzu na BMH.
Kwa upande wake, Dkt. Henry Humba kiongozi wa msafara kutoka BMH amepongeza ushirikiano uliotolewa na uongozi pamoja na wataalamu wa Hospitali ya Mzuzu, akisema umewezesha timu ya BMH kutekeleza jukumu lake kwa ufanisi, ambapo wagonjwa 576 wamehudumiwa, wagonjwa 28 wamefanyiwa upasuaji na wagonjwa 27 wamepewa rufaa kwenda BMH kwaajili ya kufanyiwa upandikizaji uloto. Ameahidi kuwa BMH itaendelea kuimarisha ushirikiano, hususan katika maeneo ya ubobezi, ili kuongeza fursa za kubadilishana ujuzi na kuhakikisha wananchi wa pande zote mbili wanapata huduma bora za afya.
Kambi hiyo imehitimishwa Hospitali ya Mzuzu, kuanzia Tarehe 5 hadi 9/10/2026 itakuwa Hospitali ya Kamuzu iliyopo Lilongwe, kambi hii imedhaminiwa na Azam, MSD, Petroda, Meru na SOTAC





No comments:
Post a Comment