KADOGOSA AAGIZA BARABARA YA MOROGORO–DUMILA–DODOMA KUPITIKA WAKATI WOTE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, October 11, 2026

KADOGOSA AAGIZA BARABARA YA MOROGORO–DUMILA–DODOMA KUPITIKA WAKATI WOTE


Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imeelekeza kuimarishwa kwa maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua katika barabara ya Morogoro–Dumila–Dodoma, hususan eneo la Daraja la Mkundi wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, ili kuhakikisha barabara hiyo inaendelea kupitika wakati wote, hata katika kipindi cha mvua kubwa na mafuriko.

Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, wakati wa ziara ya kukagua utayari wa miundombinu ya barabara hiyo kukabiliana na athari za mvua.

Daraja la Mkundi ni kiungo muhimu cha usafirishaji wa bidhaa na watu kutoka bandarini kwenda mikoa mbalimbali ya Tanzania pamoja na nchi jirani za Rwanda na Burundi,

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Waziri Kadogosa amesema ni muhimu kuchukua tahadhari mapema kwa kubaini maeneo hatarishi na kuandaa njia mbadala zitakazotumika endapo mvua kubwa au mafuriko yataathiri upitishaji wa magari.

“Kuchukua tahadhari mapema ni jambo la msingi, msisubiri hadi madhara yatakapojitokeza, andaeni njia mbadala zitakazotumika endapo hali ya barabara itakuwa ngumu kutokana na mvua au mafuriko,” amesema Kadogosa.

Amesema hatua zinazopaswa kuchukuliwa ni pamoja na kubaini maeneo yanayoweza kusababisha magari kukwama, kurekebisha sehemu zenye changamoto na kuandaa njia za mchepuko ili kuhakikisha magari yanaendelea na safari hata pale daraja litakaposhindwa kupitika.

Kadogosa pia amesisitiza umuhimu wa kuharakisha maandalizi ya ujenzi wa daraja jipya katika eneo hilo, akieleza kuwa barabara hiyo ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi na usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi jirani.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amewataka wataalamu wote wanaohusika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa wakati, akisisitiza kuwa utayari wa miundombinu na usimamizi madhubuti wa usafiri ni muhimu katika kulinda maisha ya wananchi, kuendeleza shughuli za kiuchumi na kuhakikisha magari yanaendelea kupita katika barabara hiyo.


Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Baraka Mwambage, amesema daraja hilo lilijengwa mwaka 1980 na kwa muda mrefu limekuwa likikabiliwa na changamoto ya mkusanyiko wa mchanga katika eneo la daraja, hasa wakati wa mvua.

Amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua za muda mfupi za kuondoa mchanga ili kuruhusu maji kupita na kupunguza hatari ya mafuriko.

"Kwa mwaka huu, hatua hizo zimeendelea kutekelezwa, ikiwemo uchimbaji wa mchanga katika eneo lenye urefu wa takribani mita 500. Kati ya eneo hilo, mita 400 zipo upande wa chini wa mkondo wa maji (downstream), huku kazi zikiendelea katika sehemu iliyobaki", amesema Mhandisi Mwambage.

No comments:

Post a Comment