Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, ametoa kibali kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) kutangaza zabuni ya kumpata mkandarasi atakayejenga barabara ya Nyololo–Mtwango yenye urefu wa kilomita 42 kwa kiwango cha lami, mkoani Iringa.
Kibali hicho kimetolewa wakati wa ziara ya kikazi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, baada ya kusikiliza changamoto mbalimbali na kuzungumza na wananchi wa Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani humo.
“Najua miezi mitano iliyopita Waziri Mkuu alipita hapa na akasema katika zile kilomita 42, kilomita 20 zitangazwe. Na leo tena Makamu wa Rais amefika hapa, sasa natoa kibali hapa hapa. Sihitaji Mtendaji Mkuu uniletee ofisini, katangazeni barabara hiyo,” alisema Kadogosa.
Hatua hiyo inalenga kuharakisha mchakato wa kumpata mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo, ambayo imekuwa ikihitajika kwa muda mrefu na wananchi wa Mufindi.
Katika hatua nyingine, Waziri Kadogosa alisema Serikali tayari imemlipa mkandarasi wa barabara ya Mafinga–Mgololo malipo ya awali ili kuanza utekelezaji wa mradi huo na hivi sasa mkandarasi anaendelea na maandalizi ya awali ya mradi (mobilisation) kabla ya kuanza kwa kazi za ujenzi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mufindi Kusini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, aliishukuru Wizara ya Ujenzi kwa kupokea na kutekeleza maelekezo ya viongozi wakuu wa Serikali kuhusu ujenzi wa barabara ya Nyololo–Mtwango.
Kihenzile alisema barabara hiyo imekuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa Mufindi, hivyo hatua ya kuidhinisha kutangazwa kwa zabuni ni muhimu katika kufanikisha matarajio yao ya kupata barabara ya lami.







No comments:
Post a Comment