
Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola, amezindua rasmi kambi ya matibabu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), inayofanyika katika Hospitali ya Mzuzu Central nchini Malawi, kambi hii ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa diplomasia ya afya kati ya Tanzania na Malawi. Kambi hiyo inatoa huduma za kibingwa katika tiba na upasuaji wa mifupa, magonjwa ya mfumo wa fahamu, figo, selimundu pamoja na magonjwa ya mfumo wa mkojo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Balozi Kayola amesema uwepo wa kambi hiyo unaendeleza uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Malawi, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia madaktari bingwa wa BMH kuleta huduma hizo nchini Malawi. Ameongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Afya pamoja na wadau mbalimbali, ikiwemo MSD, TPA, Petroda na Meru Oil, wamekuwa na mchango muhimu katika kufanikisha kambi hiyo.
Kambi hiyo ilianza Septemba 28, 2026, na hadi sasa jumla ya wagonjwa 192 wamepatiwa huduma na wagonjwa 9 wamefanyiwa upasuaji mkubwa. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Usafi nchini Malawi, Dkt. Dan Namarika, ameipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa na MSD kwa kuwezesha upatikanaji wa madaktari bingwa pamoja na dawa, akieleza kuwa hatua hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi wa Malawi kupata huduma za kibingwa, sambamba na kujenga uwezo wa wataalamu wa afya wa nchi hizo mbili.
Baada ya kambi hiyo ya Mzuzu, kambi ya pili ya matibabu inatarajiwa kufanyika katika Hospitali ya Kamuzu Central, Lilongwe, kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026. Wananchi wa Malawi wametakiwa kutumia fursa hiyo kujitokeza kupata huduma za kibingwa zitakazotolewa na madaktari kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa.






No comments:
Post a Comment