Na Mwandishi Wetu - RUKWA
Ofisi ya Madini Mkoa wa Rukwa imetoa leseni 74 za uchimbaji mdogo wa dhahabu katika Wilaya ya Nkasi, huku maombi mengine 366 yakichakatwa, hatua inayolenga kuwawezesha wachimbaji wadogo na vijana kunufaika na rasilimali za madini na kuchochea uwekezaji mkoani humo.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Joseph Kumburu, amesema hayo alipokuwa akizungumza na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania, CP Awadh Juma Haji, alipotembelea banda la Ofisi hiyo katika Maonesho ya Wiki ya Vijana yanayofanyika kuanzia Oktoba 8 hadi 14, 2026.
Mhandisi Kumburu amesema leseni hizo zimetokana na eneo la kilomita za mraba 420 lililotengwa kwa ajili ya utafiti na uchimbaji wa dhahabu katika vijiji vya Nchenje, Chonga, Isale na Nkandasi, Wilaya ya Nkasi.
Ameeleza kuwa kati ya leseni zilizotolewa, 24 zimenufaisha wanawake, huku maombi mengine 366 yakiendelea kuchakatwa, yakiwemo maombi 86 ya leseni na maombi 15 yaliyowasilishwa na vyama, jumuiya na taasisi mbalimbali zinazolenga kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za uchimbaji wa madini.
Aidha, amesema Ofisi hiyo inashirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kupitia Kambi ya 846 KJ Luwa, kufanya utafiti wa dhahabu katika Kijiji cha Luwa ili kubaini fursa zaidi za uchimbaji na uwekezaji.
Amesema Mkoa wa Rukwa, unaotajwa kuwa Sleeping Giant of Mineral Resources, una zaidi ya aina 100 za madini, yakiwemo ya metali kama shaba, titanium, bati, chuma na dhahabu; madini ya vito kama rubi, zumaridi, garnet, aquamarine, tourmaline na kyanite; pamoja na madini ya viwandani kama mica na feldspar. Mkoa huo pia una rasilimali za helium, lithium, makaa ya mawe na madini ya ujenzi.
Katika hatua nyingine, Kumburu amesema Mkoa wa Rukwa umetenga ekari 2,000 katika Kata ya Mkangale, Namanyere, Wilaya ya Nkasi, kwa ajili ya maandalizi ya Kongani ya Viwanda vya Madini ya Shaba (Copper Mineral Industrial Park).
Ameeleza kuwa katika maandalizi ya mradi huo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Madini imetenga maeneo 26 yenye viashiria vya shaba kwa ajili ya utoaji wa leseni za utafiti chini ya usimamizi wa Tume ya Madini, hatua inayolenga kuwawezesha wawekezaji kupata maeneo ya kufanya utafiti na uchimbaji wa madini hayo.
Amesema utekelezaji wa mradi huo utaratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA).
Kwa mujibu wa Kumburu, kongani hiyo inatarajiwa kuchochea uchakataji na uongezaji thamani wa madini ya shaba, kuvutia uwekezaji, kuongeza fursa za ajira na kukuza mapato ya Serikali.
Akitoa pongezi baada ya kutembelea banda hilo, CP Awadh ameipongeza Tume ya Madini, hususan Ofisi ya Madini Mkoa wa Rukwa, kwa juhudi za kufanya utafiti wa awali na kuibua fursa za madini, akibainisha kuwa wananchi wengi bado hawafahamu utajiri wa rasilimali za madini zilizopo mkoani humo.
Maonesho ya Wiki ya Vijana yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 14, 2026, sambamba na kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru.



No comments:
Post a Comment