
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Serikali imeielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (TIRA) kuendelea kuhakikisha wananchi wanatumia bima kwani ni sehemu muhimu ya juhudi za kujenga uchumi imara, jumuishi na endelevu.
Maelekezo hayo yametolewa Oktoba 16, 2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde wakati akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika hafla ya Uzinduzi wa Ripoti ya Utendaji wa Soko la Bima 2025.
Naibu Waziri ameeleza kuwa sehemu kubwa ya wananchi bado hawajajua na hawajawa na uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa bima, namna ya kupata huduma za bima na namna ya kufuata taratibu za kudai fidia hivyo, pamoja na TIRA kuhakikisha wananchi wanatumia bima, pia taasisi iendelee kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha elimu ya bima inawafikia wananchi katika maeneo yote nchini.
"Tunataka kuona soko la bima lenye ushiriki mkubwa wa watu wa kati ili kuongeza ajira, kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi pamoja na kukuza ujuzi hivyo, serikali itaendelea kuhakikisha kuwa maslahi ya wateja wa huduma za bima yanalindwa na mwenendo wa watoa huduma za bima unasimamiwa kwa ueledi na haki kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo", amesema Mhandisi Munde.
Ameongeza kuwa, serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kisera ili kuhakikisha ukuaji thabiti wa sekta ya bima iliyo jumuishi na inayotoa mchango madhubuti katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa.
Amemalizia kwa kutoa rai kwa TIRA kuendelea kuwa chachu ya ustawi wa maendeleo ya soko la bima kwa kuhamasisha uwekezaji na kulinda haki za wateja na kuifanya sekta ya bima iendane, iaminiwe na kusaidia wananchi wote kwani katika uchumi unaokua kwa kasi kama wa nchi ya Tanzania, umuhimu wa bima unaendelea kuongezeka.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Hamad Omar Bakari amewasisitiza TIRA kuendelea kusimamia kwa karibu mwenendo wa makampuni ya bima na watoa huduma wengine ili kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni, miongozo na viwango vya huduma vinavyowekwa.
"Tumekuwa tukitoa maelekezo ya mara kwa mara kwa makampuni ya bima kuendelea kuboresha huduma kwa wateja hususan katika eneo la ufuatiliaji wa madai. Tukijenga imani kwa wananchi, wananchi wengi zaidi wataona umuhimu wa kuwa na bima na hivyo kuongeza ushiriki wao katika soko la bima", amesema Dkt. Bakari.
Akitoa taarifa ya utendaji wa soko la bima nchini, Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware amesema kuwa, soko hilo limeendelea kukua kwa kasi likipanua wigo wa huduma na kuongeza mchango wake na ustawi wa wananchi ambapo kati ya mwaka 2024 hadi 2025, mtaji halisi umeongezeka kutoka shilingi bilioni 697.4 hadi shilingi trillion 1.89, uwekezaji umeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.41 hadi shilingi trilioni 2.24, wakata bima na wanufaika wameongezeka kutoka watu milioni 25.9 mwaka 2024 hadi watu milioni 26.8 mwaka 2025 huku wakatabima wakiwa milioni 8.7 na wanufaika milioni 18.1.
"Watoa huduma za bima wameongezeka kutoka
1,741 mwaka 2024 hadi 10,940 mwaka 2025, ajira katika sekta ndogo ya bima iliongezeka kutoka 6,434 mwaka 2024 hadi 15,398 mwaka 2025, ada za bima zimeongezeka kutoka shilingi trillioni 1.52
mwaka 2024 hadi shilingi trilioni 2.55 mwaka 2025, mali za bima zimeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.14 hadi shilingi trilioni 4.06 mwaka 2025", amemalizia Dkt. Saqware.


No comments:
Post a Comment