TANZANIA NA BENKI YA DUNIA ZAWEKA MKAKATI WA PAMOJA KUCHOCHEA MAGEUZI YA UCHUMI NA KUTENGENEZA AJIRA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 14, 2026

TANZANIA NA BENKI YA DUNIA ZAWEKA MKAKATI WA PAMOJA KUCHOCHEA MAGEUZI YA UCHUMI NA KUTENGENEZA AJIRA


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kushoto) akiwa katika picha na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Uendeshaji, Bi. Anna Bjerde, mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini Bangkok nchini Thailand, ambapo walijadili mikakati ya kuharakisha maendeleo ya uchumi wa Tanzania, hususan katika maeneo ya ujenzi wa miundombinu, uandaaji wa ajira na uhamasishaji wa uwekezaji wa sekta binafsi.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kushoto) akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Uendeshaji, Bi. Anna Bjerde, mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini Bangkok nchini Thailand, ambapo walijadili mikakati ya kuharakisha maendeleo ya uchumi wa Tanzania, hususan katika maeneo ya ujenzi wa miundombinu, uandaaji wa ajira na uhamasishaji wa uwekezaji wa sekta binafsi.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Katikati), Waziri wa Fedha-Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil (Mb) (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (wa pili kulia), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Dkt. Tausi Kida (kulia), na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Robert Mtengule, wakiwa katika kikao na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Uendeshaji, Bi. Anna Bjerde, mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini Bangkok nchini Thailand, ambapo walijadili mikakati ya kuharakisha maendeleo ya uchumi wa Tanzania, hususan katika maeneo ya ujenzi wa miundombinu, uandaaji wa ajira na uhamasishaji wa uwekezaji wa sekta binafsi.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Bangkok, Thailand)


Na Benny Mwaipaja, Bangkok, Thailand


Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amekutana na viongozi wa Benki ya Dunia jijini Bangkok, Thailand, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, inayofanyika nchini humo, kujadili mikakati ya kuharakisha maendeleo ya uchumi wa nchi, hususan katika maeneo ya ujenzi wa miundombinu, uandaaji wa ajira na uhamasishaji wa uwekezaji wa sekta binafsi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Balozi Omar amesisitiza umuhimu wa kuelekeza jitihada za maendeleo kutoka katika kupima mafanikio kwa viashiria vya ukuaji wa uchumi pekee, badala yake izingatie matokeo halisi yanayogusa maisha ya wananchi, ikiwemo kuongeza uzalishaji, kupanua fursa za ajira na kuinua kipato.

Sekta ya utalii pia ilitajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira kwa haraka na kuchochea shughuli za kiuchumi. Mhe. Balozi Omar alieleza kuwa licha ya Tanzania kuwa na vivutio vingi vya utalii, bado kuna fursa ambazo hazijatumika kikamilifu, hususan katika maeneo yanayozunguka maziwa makubwa na ukanda wa pwani.

Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza maeneo hayo ili kuongeza idadi ya watalii, kupanua wigo wa shughuli za kiuchumi na kufungua fursa zaidi za ajira kwa wananchi.

Aidha, mkutano huo ulijadili umuhimu wa Ushoroba wa Kati (Central Corridor) kama moja ya miundombinu muhimu ya usafirishaji inayoweza kuimarisha biashara ya kikanda, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuunganisha masoko ya Tanzania na nchi jirani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Uendeshaji, Bi. Anna Bjerde, alisisitiza kuwa uandaaji wa ajira ndio kipaumbele kikuu cha Benki hiyo katika juhudi za kuchochea maendeleo ya Uchumi, na kwamba Benki ya Dunia inaendeleza mkakati huo unaolenga kuimarisha biashara ndogo, za kati na ndogo sana (MSMEs), ambazo zinachangia sehemu kubwa ya biashara na ajira katika uchumi.

Katika kufanikisha azma hiyo, viongozi hao walijadili umuhimu wa kuboresha mifumo ya upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo, kwa kuhamia kutoka mfumo unaotegemea zaidi dhamana za mali kwenda kwenye tathmini ya mtiririko wa fedha za biashara, hatua inayolenga kuwezesha biashara kupata mitaji kulingana na uwezo wake wa kuzalisha mapato, kukua na kuongeza ajira.

Aidha, aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kuweka mkazo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, hususan kupitia sekta za kilimo, mifugo na uongezaji thamani ya madini, akibainisha kuwa mkakati huo unalenga kuongeza manufaa ya rasilimali za nchi kwa kuhakikisha sehemu kubwa zaidi ya thamani ya bidhaa inazalishwa ndani ya nchi, ili kufikia asilimia 40 ya lengo la uongezaji thamani.

Katika sekta ya elimu, Bi. Bjerde alisisitiza umuhinu wa kuimarisha ubora wa elimu na matokeo ya ujifunzaji, badala ya kuzingatia ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule pekee, huku Benki ya Dunia ikisisitiza haja ya kuboresha mbinu za ufundishaji na mifumo ya elimu kwa kutimia mifumo midogo ya Akili Unde ili kuwaandaa vijana kukabiliana na mabadiliko ya uchumi wa dunia na mahitaji ya soko la ajira.

Kuhusu ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, viongozi wa Benki ya Dunia walieleza dhamira ya taasisi hiyo ya kuongeza kasi na ufanisi katika maandalizi na utekelezaji wa miradi kwa kupunguza muda unaotumika kuandaa miradi kabla ya kuanza kutekelezwa.

Aidha, Benki hiyo inaandaa mpango maalumu wa kuharakisha utekelezaji wa miradi kwa kubaini na kuondoa vikwazo vinavyochelewesha maendeleo yake.

Kwa upande wa Tanzania, viongozi waliohudhuria kikao hicho walieleza dhamira ya kuendeleza ushirikiano huo kwa kuimarisha ufanisi wa utekelezaji wa miradi na kutumia ipasavyo nyenzo za kifedha zinazolenga kusaidia mageuzi ya uchumi.

Mkutano huo ulihitimishwa kwa pande zote mbili kukubaliana kuendeleza ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Benki ya Dunia ili kuharakisha utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya nchi.

Benki ya Dunia pia ilihimiza Serikali ya Tanzania kuendelea kuwasilisha mahitaji yake ya maendeleo kwa ujasiri, ili fursa za ushirikiano na msaada ziweze kutumika ipasavyo katika kufanikisha malengo ya kitaifa.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, Waziri wa Fedha-Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Dkt. Tausi Kida, na Maafisa wengine waandamizi wa Serikali na Benki ya Dunia.






No comments:

Post a Comment