
Kamati ya Pamoja ya Ufundi kati ya Tanzania na Uganda (Joint Technical Committee) imekutana jijini Tanga, katika eneo la Chongoleani, kwa ajili ya kumkabidhi Mshauri Mwelekezi kutoka kampuni ya Worley Consulting Group Limited eneo linalotarajiwa kujengwa miundombinu ya kupokelea, kuhifadhi na kusafirisha mafuta yaliyosafishwa.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda katika kuendeleza miradi ya kimkakati katika sekta ya nishati. Makabidhiano hayo yatamwezesha Mshauri Mwelekezi kuanza kazi za awali za upembuzi yakinifu, ikiwemo upimaji wa udongo, tathmini ya mazingira na usanifu wa awali wa miundombinu hiyo.
Miundombinu hiyo inatarajiwa kuongeza thamani katika mnyororo wa mafuta ghafi yatakayopita kupitia bomba la EACOP, huku ikichangia kupunguza utegemezi wa uagizaji wa mafuta yaliyosafishwa, kuimarisha usalama wa upatikanaji wa bidhaa za petroli na kuongeza fursa za biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Kamishna Msaidizi wa Mkondo wa Kati na Chini wa Petroli kutoka Wizara ya Nishati, Grace Mwakasege, amesema mradi huo ni wa kimkakati na unatarajiwa kuchangia katika kuifanya Tanga kuwa kitovu muhimu cha shughuli za mafuta na gesi katika ukanda wa Afrika Mashariki.







No comments:
Post a Comment