RUKWA, Oktoba 2026 – Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewahimiza vijana wajasiriamali nchini kuzingatia viwango na ubora wa bidhaa wanazozalisha ili kuongeza ushindani katika soko na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana nchini na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa na Afisa Masoko Mwandamizi wa TBS, Deborah Haule, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua mkoani Rukwa, ambapo TBS inashiriki kutoa elimu kuhusu viwango, ubora na usalama wa bidhaa.
Bi. Haule amesema maadhimisho hayo yamekuwa fursa muhimu kwa TBS kukutana na vijana, hususan wajasiriamali, kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango katika uzalishaji na kuwafahamisha huduma zinazotolewa na Shirika ili kuwawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.
Ameeleza kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kuwawezesha vijana wajasiriamali wanaostahili kupata huduma ya upimaji wa sampuli za bidhaa bila malipo, kwa lengo la kuwasaidia kutambua ubora wa bidhaa zao na kuboresha uzalishaji.
“Tunawahimiza vijana wajasiriamali wenye bidhaa wanazozalisha kutumia fursa hii kwa kufika katika ofisi za TBS ili kupata maelekezo na huduma zinazowawezesha kuthibitisha ubora wa bidhaa zao,” amesema Bi. Haule.
Aidha, amesema maabara za TBS zinafanya kazi kwa kuzingatia mahitaji ya umahiri wa kimataifa, jambo linalosaidia kuhakikisha matokeo ya vipimo yanaaminika na kukubalika kulingana na taratibu na makubaliano husika.
Ameongeza kuwa TBS ina ofisi katika kanda mbalimbali nchini zinazotoa huduma na elimu kuhusu viwango, hivyo kuwataka vijana kuendelea kutembelea ofisi hizo hata baada ya kumalizika kwa maadhimisho hayo ili kupata ushauri na mwongozo kuhusu ubora wa bidhaa na huduma za Shirika.
Akizungumzia kaulimbiu ya maadhimisho hayo, “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana,” Bi. Haule amesema TBS inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha vijana wanapata elimu inayowawezesha kuzingatia viwango, ubora na usalama wa bidhaa wanapochangamkia fursa za biashara na ujasiriamali.





No comments:
Post a Comment