Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) imeendelea kutoa elimu na kusimamia hatua mbalimbali za kulinda afya ya mimea, kudhibiti visumbufu na kuhakikisha mazao yanayozalishwa na kuingia nchini yanakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
Akizungumza jijini Tanga katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayoendelea kuanzia Oktoba 10 hadi 16, Saumu Zuberi Mwessongo, Afisa Kilimo kutoka TPHPA, Kitengo cha Usafi wa Mimea na Karantini, amesema mamlaka hiyo hukagua mazao yanayoingia na kutoka nchini ili kuzuia kuenea kwa wadudu na magonjwa vamizi ambayo hayapo nchini.

Mwessongo amesema TPHPA hutumia teknolojia mbalimbali, ikiwemo ndege nyuki (drone), kufuatilia mashamba na kubaini maeneo yaliyoathirika na wadudu au magonjwa ya mimea. Aidha, mamlaka hiyo hutoa elimu kwa wakulima kuhusu uchaguzi na matumizi sahihi ya viuatilifu vilivyosajiliwa ili kulinda mazao na afya za walaji.

Ameeleza kuwa mamlaka hiyo pia hutoa vibali vya usafi wa mimea kwa mazao yanayoingizwa nchini na yale yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi. Amesema kupitia ukaguzi wa shehena za mazao, TPHPA huchukua hatua za kuzuia kuingia nchini kwa mazao yaliyobainika kuwa na wadudu au magonjwa vamizi, huku ikitoa maelekezo ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa pale changamoto zinapobainika.

Kwa upande wake, Letan Kurenia Mollel, mtaalamu kutoka Kitengo cha Hifadhi ya Taifa ya Mimea (National Herbarium of Tanzania), amesema kitengo hicho hukusanya sampuli za mimea na kufanya utambuzi wa kisayansi ili kubaini aina zake, hasa mimea isiyofahamika ambayo inaweza kuwa vamizi.
Mollel amesema mimea vamizi inaweza kuenea kwa kasi na kuathiri uzalishaji wa mazao kwa kushindana na mimea ya chakula, hali inayoweza kupunguza mavuno ya wakulima. Pia, mimea hiyo inaweza kuathiri maeneo ya malisho kwa kuenea na kuchukua nafasi ya mimea inayoliwa na mifugo na wanyamapori, hivyo kuathiri upatikanaji wa chakula cha mifugo.
Amesema utambuzi wa mapema wa mimea vamizi ni muhimu ili kuwezesha hatua za udhibiti kuchukuliwa kabla haijaenea na kusababisha madhara makubwa kwa kilimo na mazingira. Juhudi hizo zina mchango katika kulinda uzalishaji wa chakula na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Naye, Mapulish D. Hebel kutoka Kitengo cha Teknolojia za Vinyunyizi vya Viuatilifu cha TPHPA amesema mamlaka hiyo husimamia usajili na ukaguzi wa vifaa vya kunyunyizia viuatilifu vinavyoingia nchini ili kuhakikisha vinakidhi vigezo vya ubora na vinafaa kwa matumizi ya kilimo.
Hebel amesema mamlaka hiyo pia hutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu, namna ya kudhibiti visumbufu vya mimea na mbinu bora za kunyunyizia dawa. Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza tija na kupunguza madhara ya viuatilifu kwa afya ya binadamu na mazingira.
Kwa upande wake, Masoud Matimbwa kutoka Kitengo cha Kudhibiti Visumbufu vya Mlipuko cha TPHPA amesema mamlaka hiyo imefanikiwa kudhibiti kwelea kwelea kwa kiwango kikubwa katika maeneo ya Babati, Moshi, Pwani na Kilosa, hatua inayosaidia kulinda mazao ya wakulima na kuongeza kipato chao.
Matimbwa amewataka wakulima kukagua mashamba yao mara kwa mara na kutoa taarifa mapema wanapobaini dalili za uvamizi wa visumbufu vya mimea ili hatua za udhibiti zichukuliwe kabla havijasababisha uharibifu mkubwa wa mazao. Amesema utambuzi wa mapema utasaidia kuokoa mazao na kuongeza tija katika uzalishaji wa chakula.
Akizungumza, Alfred Kiraho, mtaalamu kutoka Idara ya Usimamizi wa Viuatilifu ya TPHPA, amewashauri wafanyabiashara wanaosafirisha mazao nje ya nchi kupeleka sampuli maabara kupima masalia ya viuatilifu kabla ya kusafirisha, na hatua hiyo husaidia kuhakikisha mazao yanakidhi viwango vya usalama vinavyotakiwa katika masoko ya kimataifa, huku majibu ya maabara hiyo yakiaminika na kukubalika duniani.


No comments:
Post a Comment