UJENZI WA BARABARA YA LUSAHUNGA - RUSUMO WAFIKIA ASILIMIA 69 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, October 2, 2026

UJENZI WA BARABARA YA LUSAHUNGA - RUSUMO WAFIKIA ASILIMIA 69


Ujenzi wa barabara ya Lusahunga–Rusumo yenye urefu wa kilomita 92 umefikia asilimia 69, huku Serikali ikieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachochea usafirishaji wa watu na bidhaa na kuongeza shughuli za kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Barabara hiyo ni sehemu muhimu ya mtandao wa barabara wa Afrika Mashariki unaoiunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Mhandisi Emmanuel Luchemba kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Kagera, amesema barabara hiyo ni kiungo muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa kati ya Tanzania na nchi hizo.

Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutaimarisha shughuli za uzalishaji, hususan katika sekta za kilimo, biashara, usafirishaji na uchimbaji wa madini, kwa kuwezesha mazao, bidhaa na rasilimali nyingine kusafirishwa kwa ufanisi zaidi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Luchemba, mradi huo pia utasaidia kupunguza gharama za usafirishaji na kuboresha upatikanaji wa masoko ya ndani na ya kikanda.

Kutokana na umuhimu wa barabara hiyo, Serikali inaijenga upya kwa kiwango cha lami kinachoweza kuhimili magari mazito, huku ikitumia usanifu wa kisasa wa tabaka la lami unaojulikana kama Superpave.

Amesema matumizi ya usanifu huo yanalenga kuongeza uimara wa barabara, kupunguza gharama za matengenezo na kuimarisha usalama wa watumiaji.

Mhandisi Luchemba amesema mradi huo ulianza Julai 5, 2023 na unatarajiwa kukamilika Desemba 10, 2026. Unatekelezwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kutoka China, huku huduma za ushauri wa uhandisi zikitolewa na Kampuni ya NORPLAN Tanzania Limited kwa ubia na TYPSA.

“Mradi huu ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa chini ya Programu ya Tanzania Transport Integration Project (TanTIP), inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri na kuongeza ufanisi wa mtandao wa barabara nchini,” amesema Mhandisi Luchemba.

Amebainisha kuwa hadi sasa, ujenzi wa makalavati madogo, makalavati makubwa (Box Culverts) na tabaka la udongo G15 umekamilika kwa asilimia 100.

“Ujenzi wa tabaka la udongo lililoimarishwa kwa saruji (CM) umefikia asilimia 95, sawa na kilomita 88, huku ujenzi wa tabaka la msingi kwa kiwango cha Superpave 37.5 ukifikia asilimia 84.2, sawa na kilomita 77.12 kwa tabaka la kwanza,” amefafanua.

Ameongeza kuwa ujenzi wa tabaka la pili umefikia asilimia 58.3, sawa na kilomita 54.7. Kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa njia za magari yanayopanda (Climbing Lanes) pamoja na njia za watembea kwa miguu katika vituo vyote vya mradi, zenye urefu wa jumla ya kilomita 20.

Mradi huo unatarajiwa kuimarisha muunganiko wa usafiri na biashara kati ya Tanzania na nchi jirani, sambamba na kuweka mazingira bora ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment