Na: OWM–TAMISEMI, Iringa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amewaelekeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuhakikisha wakulima wananunua mbolea kwa bei elekezi iliyowekwa na Serikali ili kuwapunguzia gharama za uzalishaji na kuwaongeza mavuno na kipato.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo, Oktoba 18, 2026, akiwa Iringa katika mkutano wa hadhara, baada ya kupewa fursa na Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, kueleza hatua zinazochukuliwa na Serikali kuwahudumia wananchi wakati wa ziara ya Makamu wa Rais ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani humo.
“Tumekubaliana na Waziri wa Kilimo kuwa yatawekwa mabango ya bei elekezi ya mbolea katika maeneo husika, na bei hiyo ndiyo itakayotumiwa na wafanyabiashara kuwauzia wakulima. Hivyo, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wasimamie utekelezaji wa maelekezo hayo,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, amempongeza Prof. Shemdoe kwa maelekezo hayo na kuwataka viongozi hao kuhakikisha usimamizi unafanyika katika maeneo yao ya utawala badala ya kukaa ofisini, ili wakulima wanunue mbolea kwa bei elekezi.
“Kama Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala Wilaya, Afisa Tarafa, Mtendaji wa Kata na Mtendaji wa Kijiji hawatasimamia kikamilifu bei elekezi, hata yakiwekwa mabango bado mkulima ataumizwa na bei ya mbolea,” amesisitiza Mhe. Ndejembi.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa usimamizi wa bei elekezi unaendana na azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha kila Mtanzania anatendewa haki katika ununuzi wa bidhaa na upatikanaji wa huduma za kijamii.
Usimamizi madhubuti wa bei elekezi za mbolea ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kumlinda mkulima, kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza tija na kipato, pamoja na kuimarisha usalama wa chakula na uchumi wa taifa.







No comments:
Post a Comment