ZUNGU: MABUNGE IMARA NI YA MAKUNDI YOTE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, October 5, 2026

ZUNGU: MABUNGE IMARA NI YA MAKUNDI YOTE



NA Mwandishi Wetu , ARUSHA


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb), amesema ongezeko la uwakilishi wa wanawake katika mabunge ni hatua inayotia moyo, lakini limewataka Mabunge Wanachama wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika uongozi na utoaji wa maamuzi.

Mhe. Zungu ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2026, wakati akifungua Mkutano wa Jukwaa la Wanawake wa IPU unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), ambapo amesema Tanzania imepiga hatua katika suala la uwakilishi wa wanawake bungeni, huku uwakilishi huo ukifikia asilimia 39.5.

“Kwa mfano, nchini Tanzania, uwakilishi wa wanawake bungeni ni asilimia 39.5,” amesema.

Hata hivyo, amesema uwakilishi pekee hautoshi, hivyo Mabunge Wanachama wa IPU yanapaswa kuendelea kushughulikia vikwazo vinavyoathiri ushiriki madhubuti, uongozi na ushawishi wa wanawake katika michakato ya kisiasa na kibunge.

Amesema Jukwaa hilo linatoa fursa muhimu kwa washiriki kubadilishana uzoefu na kujadili masuala yanayolenga kuimarisha ushiriki wa wanawake katika mchakato wa kufanya maamuzi.

“Tunapokutana hapa Tanzania, hebu tuthibitishe tena kuwa mabunge yanayoshirikisha makundi yote ni mabunge imara zaidi,” amesema.

Mhe. Zungu amesema kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu na kwa usawa katika nyanja ya kisiasa kunaimarisha taasisi za kidemokrasia na kuchangia katika kujenga utawala unaowakilisha vyema wananchi na kujali mahitaji yao.

Amewahimiza washiriki kutumia Jukwaa hilo kubadilishana uzoefu kwa uwazi, kujenga ushirikiano na kubainisha hatua madhubuti zitakazochukuliwa katika mabunge ya nchi Wanachama.

“Majadiliano haya yanapaswa kutusaidia kutoka hatua ya ahadi hadi utekelezaji wa vitendo,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa kuondoa vikwazo vya kimfumo na kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa ya kushiriki katika maamuzi kutasaidia kujenga imani katika taasisi za kidemokrasia na kufungua fursa za pamoja zinazohitajika katika kujenga dunia yenye haki na inayoshirikisha watu wote.

Ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unatarajiwa kufanyika baadaye leo jijini Arusha.







No comments:

Post a Comment