Agizo lililotolewa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, mwezi Oktoba 2026, mkoani Shinyanga, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Msalala, wilayani Kahama, limeanza kutekelezwa baada ya vifaa na mitambo ya ujenzi kuanza kurejeshwa katika maeneo ya miradi husika, hatua inayolenga kuhakikisha kazi zinaendelea kwa kasi na kukamilika kwa wakati.
Urejeshwaji wa vifaa na mitambo hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Kadogosa, aliyesisitiza umuhimu wa kuhakikisha rasilimali zote zinazohitajika katika utekelezaji wa miradi zinapatikana na kubaki katika maeneo ya kazi ili kuepusha ucheleweshaji.
Akiwa Msalala, wilayani Kahama, Waziri Kadogosa alieleza kutoridhishwa na tabia ya baadhi ya wakandarasi kuhamisha vifaa na mitambo kutoka mradi mmoja kwenda mwingine kwa lengo la kukidhi masharti ya malipo ya awali ya maandalizi ya mradi (Mobilization).
Alifafanua kuwa tabia hiyo inaweza kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati, pamoja na kuisababishia Serikali hasara kutokana na kulazimika kulipa tena gharama za usafirishaji na uletaji wa vifaa na mitambo hiyo.
Katika hatua nyingine, utekelezaji wa agizo hilo umeanza pia katika mradi wa ujenzi wa barabara ya mchepuo ya Iringa (Iringa Bypass), yenye urefu wa kilomita 7.3, ambapo hadi Oktoba 29, 2026, mkandarasi alikuwa amerejesha mitambo 41 kati ya 65 inayohitajika kwa mujibu wa mkataba, sawa na asilimia 63.
Aidha, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ulimwita mkandarasi huyo katika kikao cha kawaida cha mradi kilichopangwa kufanyika Oktoba 30, 2026, kwa lengo la kusisitiza umuhimu wa kuendelea na utekelezaji wa kazi mara baada ya kurejesha mitambo hiyo.






No comments:
Post a Comment