BoT NA IMF ZAFANYA TATHMINI YA UTHABITI WA SEKTA YA FEDHA TANZANIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, November 21, 2026

BoT NA IMF ZAFANYA TATHMINI YA UTHABITI WA SEKTA YA FEDHA TANZANIA


Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kushirikiana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), zimefanya Tathmini ya Uthabiti wa Sekta ya Fedha kuanzia tarehe 9 hadi 20 Novemba 2026, kwa lengo la kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, udhibiti na usimamizi wa sekta ya fedha nchini.

Tathmini hiyo, iliyofuatia tathmini ndogo iliyofanyika Septemba 2026, ilihusisha wataalamu kutoka IMF, BoT, mamlaka za usimamizi wa sekta ya fedha, benki za biashara na wadau wengine. Mijadala ilijikita katika maeneo matano, yakiwemo uchambuzi na udhibiti wa vihatarishi vya kimfumo, usimamizi wa sekta ya benki, mifumo ya malipo na huduma za kifedha za kidijitali, takwimu za sekta ya fedha na usimamizi wa vihatarishi.

Akizungumza na ujumbe wa IMF katika kikao kilichofanyika BoT jijini Dar es Salaam, Novemba 20, 2026, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, alisema sekta ya fedha nchini inaendelea kukua na kubadilika kutokana na kuongezeka kwa ujumuishaji wa kifedha, matumizi ya teknolojia za kidijitali na maboresho ya mifumo ya malipo na sera za udhibiti. Alibainisha kuwa sekta hiyo ni kichocheo muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa kubaini, kutathmini na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kuathiri uthabiti wa sekta ya fedha, hususan vinavyotokana na mwingiliano wa taasisi za fedha, teknolojia na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, alieleza hatua zinazochukuliwa na BoT kuboresha usimamizi wa mabenki, mifumo ya malipo na maandalizi ya kukabiliana na migogoro ya kifedha.

Pia alisisitiza umuhimu wa Jukwaa la Uthabiti wa Sekta ya Fedha Tanzania (TFSF) katika kuratibu ushirikiano na kubadilishana taarifa miongoni mwa mamlaka za usimamizi na wadau wengine.

Timu ya IMF iliwasilisha taarifa ya awali ya tathmini yenye matokeo na mapendekezo yatakayotumika kuandaa Ripoti ya Tathmini ya Uthabiti wa Sekta ya Fedha (FSSR) na Mpango wa Kipaumbele wa Msaada wa Kitaalamu kwa mwaka 2027–2030.

Akihitimisha, Gavana Tutuba alieleza kuwa sekta ya fedha nchini inaendelea kuwa thabiti na yenye uwezo wa kuhimili misukosuko, huku akithibitisha dhamira ya BoT ya kuendelea kushirikiana na IMF kutekeleza maboresho yatakayopendekezwa.

No comments:

Post a Comment