Serikali imesema inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za njia nne kuanzia eneo la Rwamishenye kwenda Kyakairabwa na Ibura mjini Bukoba, baada ya kukamilika kwa usanifu wa miradi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 4,2026 Bungeni jijini na Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Mjini Mhandisi Johnston Mutasingwa aliyehoji ni lini ujenzi wa barabara hizo utaanza, akieleza kuwa upembuzi yakinifu ulikuwa umekamilika.
Katika majibu yake, Mha. Kasekenya amesema barabara hizo tayari zimefanyiwa usanifu na zitaingizwa katika mipango ya bajeti ili kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.
Awali, mbunge huyo ameishukuru Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa barabara ya njia Nne kutoka Rwamishenye Roundabout hadi eneo la TRA, huku akitaka ufafanuzi kuhusu hatua zinazofuata za upanuzi wa miundombinu hiyo katika maeneo mengine ya Bukoba.


No comments:
Post a Comment