
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
CHIFU Mkuu wa kabila la Wasafwa mkoani Mbeya, Rocket Mwashinga, amemwagia sifa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, kwa namna anavyotekeleza majukumu yake ya kiuongozi, akimtaja kuwa ni kiongozi msikivu, mnyenyekevu, mwenye ushirikiano mkubwa kwa wananchi bila ubaguzi, na hasa sifa ya "kutuna".
Akizungumza wakati wa zoezi la kugawa misaada kwa wananchi walioathirika na mafuriko katika Kata ya Nzovwe, Chifu Mwashinga amesema DC Itunda ni kielelezo bora cha viongozi vijana wanaohitajika nchini.

Alisema kutokana na moyo wake wa kipekee wa kujali wananchi na kuwa tayari kusikiliza na kutatua changamoto zao bila kujikweza.
Amesema jambo kubwa linalomtofautisha Mkuu huyo wa Wilaya ni urahisi wake wa kufikika na unyenyekevu alionao, akibainisha kuwa hata katika mawasiliano ya kawaida, hatoi majibu ya majivuno wala kujionyesha kuwa yeye ni mkubwa kuliko wananchi anaowaongoza.

"Uongozi bora haupimwi kwa cheo kikubwa alichonacho mtu, bali hupimwa kwa jinsi anavyowahudumia wananchi, anavyowasikiliza na kushirikiana nao bega kwa bega kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao," alisisitiza Chifu Mwashinga.

Katika tukio hilo, Chifu Mwashinga akiwa sambamba na viongozi wengine, alishiriki kikamilifu kutoa msaada wa chakula, ikiwemo mahindi, kwa wananchi waliopata pigo kutokana na mafuriko hayo ya Nzovwe, ikiwa ni jitihada za kuwafariji na kuwasaidia kurejea kwenye maisha yao ya kawaida.
Hatimaye, Chifu huyo wa jadi amesisitiza kuwa viongozi wenye hofu ya Mungu, moyo wa huruma na utayari wa kuwatumikia wananchi ndio nguzo kuu ya maendeleo ya jamii, huku akimhimiza DC Itunda kuendelea na mfano huo huo wa uongozi unaoweka mbele utu, unyenyekevu na uzalendo wa dhati.
Mwisho

No comments:
Post a Comment