DC HANIU ATOA SIKU TANO KWA WANANCHI WA SUMA-RUNGWE KUHAMA, KUFUNGUA NJIA YA UJENZI WA BARABARA YA KATUMBA–LUPASO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, November 2, 2026

DC HANIU ATOA SIKU TANO KWA WANANCHI WA SUMA-RUNGWE KUHAMA, KUFUNGUA NJIA YA UJENZI WA BARABARA YA KATUMBA–LUPASO

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Mhe. Jafar Haniu, ametoa siku tano kwa wananchi wa Kijiji cha Suma na wote wanaoishi pembezoni mwa barabara ya Katumba–Mbambo–Tukuyu kuhama katika maeneo ya hifadhi ya barabara ili kuwezesha kuanza kwa kasi kwa shughuli za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Mhe. Haniu ametoa agizo hilo leo, Novemba 2, 2026, wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 79.4. Ziara hiyo imefanyika akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rungwe.

Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuondoa makazi na shughuli zao katika maeneo ya hifadhi ya barabara ndani ya siku tano, akionya kuwa watakaokaidi agizo hilo wataondolewa na Serikali na kutakiwa kurejesha gharama za zoezi hilo. Katika ziara hiyo, amekagua sehemu mbili za mradi zinazotekelezwa na kampuni ya China Road and Bridge Corporation (CRBC), ambazo ni Katumba–Lupaso (km 35.3) na Mbaka–Kibanja (km 20.7).

Aidha, ameitaka TANROADS Mkoa wa Mbeya kuongeza usimamizi kwa mkandarasi ili kuhakikisha kazi zinafanyika usiku na mchana na mradi unakamilika kwa wakati, akibainisha kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema mradi huo ni wa kimkakati kwa kuwa utaimarisha mawasiliano ya usafiri kati ya Wilaya ya Kyela na Rungwe, hususani katika eneo la Halmashauri ya Busokelo.

Mhandisi Bishanga ameongeza kuwa mkandarasi tayari amepewa maelekezo ya kupeleka mitambo katika eneo la mradi na kuongeza kasi ya kazi, ikiwemo kufanya kazi usiku na mchana, ili kupunguza adha wanazokumbana nazo wananchi kutokana na hali ya barabara hiyo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rungwe, Meckon Mwakipunga, ameipongeza Serikali kwa kuanza kutekeleza mradi huo, akisema ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Serikali kwa wananchi.

Amesema CCM Wilaya ya Rungwe imefurahishwa na hatua ya kuanza kwa mradi huo pamoja na ushirikishwaji wa chama katika ziara za kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM, hatua inayowezesha kufuatilia maendeleo ya miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.

Akizungumzia umuhimu wa barabara hiyo, dereva wa magari ya abiria na mtumiaji wa mara kwa mara wa barabara hiyo, Bw. Jastine Kanjeli, ameishukuru Serikali kwa kuanza kwa ujenzi huo, akieleza kuwa wananchi na madereva wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri, hasa wakati wa mvua za masika kutokana na hali ya barabara. 

No comments:

Post a Comment