WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amefanikisha zoezi la kuchangia sh. 1,074,972,600/- ikiwa ni harambee ya ununuzi wa vifaa tiba vya hospitali ya Bulongwa iliyoko wilayani Makete, mkoani Njombe.
Harambee hiyo ilifanyika leo (Jumapili, Novemba 15, 2026) katika viwanja hospitali hiyo iliyopo kijiji cha Bulongwa ambayo inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Kati Makete.
Akizungumza na waumini wa kanisa hilo, viongozi na wananchi waliohudhuria hafla ya uchangiaji, Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu ya dini katika kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi wote.
Alitumia fursa hiyo kuwafikishia salamu za pongezi kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusiana na harambee hiyo iliyolenga kuchangisha sh. bilioni moja. "Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewatakia heri katika jambo hili jema na lenye manufaa makubwa kwa wananchi wetu bila kujali dini au itikadi zao," alisema.
Mapema, Mkuu wa Dayosisi ya Kusini Kati, Askofu William B. Sanga alisema kufanyika kwa harambee hii ni udhihirisho jinsi kanisa linavyoweza kumhudumia mwanadamu kimwili na kiroho.
Akitoa historia ya hospitali ya Bulongwa, Baba Askofu Sanga alisema lilianza kutoa huduma mwaka 1944 ikiwa ni zahanati tu na mhudumu wake alikuwa akitembea umbali wa zaidi ya km 100 kutokea Itete hadi hapo.
Alisema hospitali mpya ilijengwa kati ya mwaka 1967 na 1968 na imekuwa ikihudumia wananchi mbalimbali wa Nyanda za Juu Kusini hasa kwenye tiba ya viungo bandia.
Akitoa ufafanuzi kuhusu harambee hiyo, Baba Askofu Sanga alisema wamepanga kununua vifaa tiba vipya kwa sababu hospitali ya sasa inapaswa kuhama ili kupisha ujenzi wa bwawa la umeme la mto Lumakalya.
"Watu wanajiuliza iweje tunafanya harambee ilhali tunatakiwa kuhama. Hatuhusiki na ujenzi wa miundombinu, tunahusika na ununuzi wa vifaatiba. Naomba tusichanganye, hivi vifaa ni vya hospitali mpya. Tumeshapata eneo la ekari 49.8 kutoka kijiji cha Bulongwa."
"Vifaa vya mionzi kama vile X-Ray, CT SCAN na Mammogram tayari tumeshaviagiza. Sasa hivi tunahitaji vifaa vya upasuaji na maabara. Kwa hiyo, ujenzi wa hospitali ukiisha, tunahama na vifaa vyetu na tunaanza kutoa huduma mara moja," alisema.
Naye, Mbunge wa Makete, Festo Sanga alisema Serikali imefanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo katika wilaya hiyo. "Mwaka 2020 wakati naanza ubunge, kulikuwa na vituo vya afya vitatu na leo hii chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan tumejenga vituo vipya saba."
"Wakati naanza kazi, jimbo hili lenye vijiji 98, umeme ulikuwa upo kwenye vijiji 32 tu. Leo hii, vijiji vyote 98 vina umeme. Hata kwenye elimu, shule za sekondari zilikuwa hazifiki tano, lakini leo ziko 12. Tunaishukuru Serikali imefanya kazi kubwa sana," alisema.
Ametumia fursa kuomba barabara ya kutoka Makete hadi Mbeya ijengwe kwa haraka kwa sababu imekuwa ni kilio cha muda mrefu cha wakazi wa wilaya hiyo. “Mkandarasi yupo lakini spidi yake ni ndogo sana,” alisisitiza.







No comments:
Post a Comment