Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kimewataka wahitimu wa chuo hicho kutumia elimu, ujuzi na maarifa waliyoyapata kutatua changamoto za jamii, kujiajiri na kuajiri wengine badala ya kutegemea vyeti pekee kupata ajira, kikieleza kuwa elimu inapaswa kuwa na matokeo yanayoonekana katika maisha ya wahitimu na jamii kwa ujumla.
Akizungumza Novemba 18, 2026, jijini Dodoma katika Siku ya Masajili (Convocation) ya chuo hicho, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi, Joseph Kuzilwa, amesema wahitimu wanapaswa kutumia elimu yao kwa namna inayochangia maendeleo ya taifa kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050, akisisitiza kuwa cheti si mwisho wa elimu bali ni msingi wa kutumia maarifa kujenga maisha, kujiendeleza kielimu na kuisaidia jamii.

Kuzilwa amesisitiza matumizi sahihi ya akili mnemba (AI) katika elimu, akieleza kuwa teknolojia hiyo inaweza kusaidia ufundishaji na ujifunzaji lakini pia inaweza kudhoofisha uwezo wa mtu kufikiri ikiwa itatumika vibaya, amesema matumizi yake yanapaswa kuwa jumuishi kwa kuchanganya na uwezo wao binafsi wa kitaaluma ili kupata manufaa zaidi.


Pia amewataka wahitimu waliopo kwenye maeneo ya kazi kushirikiana na chuo kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi, kuwafanyia mentorship na kuwasaidia kupata uzoefu wa mazingira halisi ya kazi, huku waajiri wakitoa mrejesho utakaosaidia kuboresha mitaala na kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hozen Mayaya, amesema chuo kimepiga hatua katika ukuaji na utoaji wa elimu, kutoka kuwa na wanafunzi 14 na watumishi takribani 13 hadi kufikia wanafunzi zaidi ya 15,000 na watumishi 495, akieleza kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya juhudi za chuo kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya taifa.

Mayaya amesema chuo kinaendelea kuimarisha kituo cha ujasiriamali na ubunifu MEI (Mipango Entrepreneurship and Innovation Centre) kwa ajili ya kuwajengea wanafunzi ujuzi wa ziada wa kujiajiri na kuajiriwa, huku kikitarajia kujenga kituo kikubwa cha ubunifu katika Kampasi ya Furaha iliyopo Mjini Dodoma kupitia mradi unaotajwa kuwa na thamani ya Sh bilioni 2.6, utakaowezesha wanafunzi na wadau wengine kupata fursa za ubunifu.
Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Dimoso, amesema kituo cha ubunifu na ujasiriamali kimeanza kuonesha matokeo kupitia wanafunzi watano wa Diploma ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) waliobuni mfumo wa kidijitali wa kupanga foleni hospitalini, unaomwezesha mgonjwa kujisajili na kupata taarifa ya namba yake pamoja na muda anaotarajiwa kumuona daktari.
Amesema mfumo huo utasaidia kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri huduma hospitalini, kwa kuwa wanaweza kuendelea na shughuli zao nyingine wakati wakisubiri muda wa kwenda kumuona daktari, huku akieleza kuwa chuo kimeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia na akili mnemba katika ufundishaji na ujifunzaji na ufaulu wa wanafunzi umeongezeka ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Katika Siku hiyo ya Masajili, chuo pia kimetambua wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo na wahadhiri waliofanya vizuri katika utafiti na machapisho ya kitaaluma, hatua inayolenga kuhamasisha ubora wa elimu, ubunifu, tafiti na matumizi ya maarifa katika kutatua changamoto za jamii.

No comments:
Post a Comment