Na Boniphace Epimack, OKULYBLOG - Dodoma
Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma kupitia Dawati la Elimu kwa Umma limewataka wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma kuzingatia usalama barabarani wakati wa likizo ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
Akizungumza na wanafunzi hao Novemba 13, wakati shule hiyo ikifunga muhula Sajenti Ester Makali kutoka Ofisi ya Kamanda wa Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma (RTO) alisema likizo si sababu ya wanafunzi kusahau sheria na kanuni za barabarani.
“Barabara ni eneo la kuwafikisha kwenye ndoto zenu, endeleeni kuzingatia kanuni na sheria za usalama barabarani,” alisema.
Kuhusu usalama wakati wa mvua, Sajenti Makali aliwataka wazazi kuwavalisha watoto mavazi yanayoonekana kwa urahisi pale wanapotumwa dukani au sehemu nyingine hasa kukiwa na mawingu na mwanga hafifu ili madereva waweze kuwaona kwa urahisi wanapovuka barabara.
Aidha, aliwasisitiza wanafunzi kuvuka barabara kwenye vivuko salama na pale wanapotumia vivuko vya kujitegemea visivyo na zebra wawe makini zaidi.
“Usikivu ni muhimu, sikilizeni miungurumo ya vyombo vya moto kabla ya kuvuka ili muweze kuvuka salama,” aliongeza.
Sajenti Makali pia aliwataka wanafunzi wasiwaogope askari polisi barabarani bali wawaombe msaada wa kuwavusha wanapohitaji.
“Ninyi ni mabalozi wa usalama barabarani mama yako na baba yako wanakutegemea sana kuweni makini ili wasije wakapelekewa taarifa kuwa umepata ajali barabarani,” alisisitiza.


No comments:
Post a Comment