MAFUNZO KWA WAZAZI NA WALEZI YALENGA KUIMARISHA HAKI NA USTAWI WA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM ZANZIBAR - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, November 21, 2026

MAFUNZO KWA WAZAZI NA WALEZI YALENGA KUIMARISHA HAKI NA USTAWI WA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM ZANZIBAR


Na Berema Suleiman Zanzibar.


Ushiriki wa wazazi na walezi katika malezi na maendeleo ya watoto wenye mahitaji maalum ni msingi muhimu katika kuhakikisha watoto hao wanapata haki zao za msingi, hususan haki ya elimu, ulinzi, malezi bora na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Hata hivyo, kufanikisha azma hiyo kunahitaji uelewa, maarifa na ushirikiano wa karibu kati ya familia, shule na jamii kwa ujumla.

Kwa kuzingatia umuhimu huo, Idara ya Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar imetoa mafunzo kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wenye mahitaji maalum, yakilenga kuwaongezea uelewa na uwezo wa kutambua, kutetea na kusimamia haki za watoto hao katika familia na jamii.

Mafunzo hayo yametolewa kupitia Mradi wa Uwezeshaji wa jamii kwa ajili ya haki na utawala bora awamu ya tano kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar ambao unalenga kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu haki za binadamu pamoja na kuwawezesha wananchi kushiriki katika kutetea na kulinda haki hizo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa mradi huo Sister Editha Asiimwe amesema upo umuhimu mkubwa wa wazazi na walezi kuwa na uelewa wa mahitaji ya watoto wenye ulemavu na mahitaji maalum, kwani watoto hao wanahitaji mazingira yanayowapa nafasi ya kujifunza, kukua na kuonesha uwezo wao bila kubaguliwa.

Alisema kuwa wazazi na walezi wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wanapata huduma zinazostahili, huku wakiepuka vitendo vya kuwaficha, kuwanyanyapaa au kuwanyima fursa kutokana na hali zao.

Ameeleza kuwa uwezeshaji wa wazazi na walezi ni hatua muhimu katika kuimarisha haki za binadamu, kwani familia yenye uelewa inaweza kuwa sehemu ya kutambua ukiukwaji wa haki na kutafuta msaada kutoka kwa taasisi zinazohusika.


Kwa upande wake, mkufunzi Nasor Haji Juma kuyoka chuo kikuu cha Zanzibar University ZU amesisitiza kuwa umuhimu wa kuwashirikisha watoto wenye mahitaji maalum katika maamuzi yanayohusu maisha na maendeleo yao hivyo ni vyema kuwapa nafasi ya kutoa maoni na kueleza mahitaji yao ni miongoni mwa sehemu ya kuheshimu utu na haki zao.

Ameongeza kuwa jamii inapaswa kubadilisha mitazamo hasi kuhusu watoto wenye mahitaji maalum na badala yake kujenga mazingira ya upendo, usawa, ushirikishwaji na kuthamini uwezo walionao.

Nae mshauri nasaha ambae Janet Ajugi ambae pia ni mkufunzi wa wa ushauri nasaha kutoka chuo kikuu cha Abdulrahman Summait Chukwani Zanzibar amesema wazazi wanapaswa kushirikiana kikamilifu katika kutatua changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu hasa katika masuala ya elimu kwani kila mtoto ana haki ya kupata elimu ambayo itamuwezesha kufikia ndoto zao katika maisha yao ya badade.

Nao baadhi ya walezi na wazazi walioshiriki katika mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo yataweza kuwasaidia wao katika malezi ya watoto wao kutokana na hali waliyonayo pamoja na kuendeleza mashirikiano yao kati yao na walimu katika kufuatilia maendeleo ya wanafunzi katika kutambua changamoto wanazokabiliana nazo na kutafuta suluhisho zinazoweza kuwasaidia kupata elimu bora.

 Wameeleza kuwa elimu waliyoipata imewaongezea uelewa kuhusu wajibu wao katika malezi, ulinzi na kusimamia haki za watoto wenye mahitaji maalum, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza maarifa hayo katika familia na jamii.

Walisema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua kuwa watoto wenye mahitaji maalum wana haki sawa na watoto wengine, hivyo wanapaswa kupewa nafasi ya kupata elimu, kushiriki katika shughuli za kijamii na kutumia vipaji na uwezo wao bila vikwazo wala ubaguzi.

Pamoja hayo wameeleza kuwa ni vyema kwa familia kuwa na nafasi kubwa kama nguzo ya kwanza ya kumjenga mtoto, ambapo wazazi na walezi wanahitajika kuwapa watoto wao upendo, ulinzi, faraja na moyo wa kujiamini ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku.

Hivyo wameiomba taasisi hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wazazi na walezi ili kuongeza uelewa kuhusu haki za watu wenye mahitaji maalum na kuimarisha ushiriki wao katika kuhakikisha watoto wanapata huduma stahiki.

Ni wazi kuwa uwezeshaji wa wazazi na walezi kwa kuwapatia maarifa sahihi unaweza kuwa chachu ya mabadiliko katika familia na jamii, na hivyo kuchangia kujenga mazingira jumuishi ambayo kila mtoto anapata nafasi ya kujifunza, kukua na kufikia ndoto zake.

No comments:

Post a Comment