
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Queen Sendiga amesema atalinda vyanzo vya maji kwa nguvu na maarifa kwa kuishirikisha jamii kuhusu uhifadhi.
Amesema katika kikao na kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira na kusisitiza hatua hiyo ni muhimu ili kupunguza gharama ya kutibu maji na kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kaimu Mwenyekiti wa kamati Mhe. Patrick Mwalunenge (Mb) amepongeza hatua hiyo na kusema vyanzo vya maji ni lazima kutunzwa ili miradi ya maji ilete matokeo katika jamii.

Amesema baada ya kukagua mto Mvuha unaochangia maji kwa asilimia 22 katika mto Ruvu mkuu na kuona uvamizi na kazi za kibinadamu zinazofanyika kinyume na taratibu.
Ameainisha kuwa kamati ya Maji na Mazingira itarudi Mvuha baada ya siku 60 kujionea hatua zilizochukuliwa.

Amepongeza ujenzi wa miundombinu ya maji iliyowezesha uwepo wa mabirika ya mifugo na matumizi ya maji nyumbani.
Miongoni mwa maeneo ya mfano huo ni Bwakira chini, mtaa wa Usukumani Morogoro vijijini ambapo serikali imejenga mabirika matano na kijiji cha Dakawa ambapo tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 225,000 limejengwa na linahudumia zaidi ya wakazi elfu sita pamoja na mifugo ambapo visima viwili vimechimbwa.

Mhe. Mwalunenge amefafanua kuwa mpango mahsusi wa kuwa na Gridi ya Taifa ya Maji unahitaji ushirikiano wa jamii .
Eneo la Ruvu ni moja ya dakio muhimu la maji katika kufanikisha azma ya serikali ya kuimarisha huduma ya majisafi kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam na Pwani, ambapo maji yake yanategemewa kujaza bwawa la Kidunda linalojengwa hivi sasa utekelezaji wake ukiwa umeshavuka asilimia 50.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeipongeza Wizara ya Maji kwa ubunifu uliofanywa na Bonde la Wami Ruvu kwa kufanikisha huduma ya majisafi kwa wananchi na mifugo, hivyo kuepusha migogoro na uhakika wa usalama wa vyanzo vya maji.

No comments:
Post a Comment