ROSE AIBUKA KUTOKA KAZI ZA NDANI HADI KUHITIMU KIDATO CHA NNE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 19, 2026

ROSE AIBUKA KUTOKA KAZI ZA NDANI HADI KUHITIMU KIDATO CHA NNE


Serikali kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) imemrejeshea matumaini ya elimu Rose Mlata (16), mkazi wa Njombe, aliyelazimika kufanya kazi za ndani baada ya kukosa msaada wa kuendelea na masomo. Kupitia elimu nje ya mfumo rasmi, Rose amehitimu kidato cha nne mwaka 2026 mkoani Morogoro na sasa ana ndoto ya kuwa mwanasheria.

Safari ya elimu ya Rose ilikwama baada ya wazazi wake kutengana, hali iliyomkosesha msaada wa kujiunga na kidato cha kwanza. Wakati wenzake wakiendelea na masomo, yeye alielekea Morogoro kutafuta kazi za ndani ili kujikimu, huku matumaini ya kutimiza ndoto zake yakianza kufifia.

Maisha yake yalichukua mwelekeo mpya alipopata kazi nyumbani kwa Stephano Nyonyo, Mwalimu Mkuu Mstaafu wa Shule ya Msingi Mwande, mkoani Morogoro. Baada ya kutambua hamu yake ya kusoma, Nyonyo alimsaidia kujiunga na Kituo cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Wamo mwaka 2022, ambako alipata fursa ya kuendelea na elimu kupitia Mradi wa SEQUIP.

Nyonyo hakumtafutia nafasi ya masomo pekee, bali alimlea kama sehemu ya familia yake na kuhakikisha anapata mahitaji muhimu hadi alipohitimu kidato cha nne. Anamwelezea Rose kuwa mtoto mwenye bidii, upendo na nidhamu, sifa zilizoimarisha uhusiano wao na kumwezesha kuendelea na masomo katika mazingira yenye faraja.

Akisimulia safari yake huku machozi yakimlengalenga, Rose anasema kurejea darasani kumemrudishia matumaini na kumjengea ujasiri wa kufikia malengo yake. Pamoja na maumivu ya changamoto za kifamilia, upendo alioupata na fursa ya elimu vimempa nguvu ya kuipigania ndoto yake ya kuwa mwanasheria na kusimamia haki.

Simulizi ya Rose inaonesha namna Serikali kupitia Mradi wa SEQUIP, kwa kushirikiana na jamii, inavyowapa nafasi ya pili vijana waliokosa fursa ya kuendelea na masomo. Kwa Rose, kuhitimu kidato cha nne ni mwanzo mpya unaompeleka karibu zaidi na ndoto yake ya kuvaa joho la uwakili.

No comments:

Post a Comment