SERIKALI YAIMARISHA ELIMU JUMUISHI, YATAKA UDONDOKAJI WA WANAFUNZI UDHIBITIWE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, November 4, 2026

SERIKALI YAIMARISHA ELIMU JUMUISHI, YATAKA UDONDOKAJI WA WANAFUNZI UDHIBITIWE



Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kuimarisha mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanapata elimu bora na fursa sawa za kujifunza, sambamba na kukabiliana na changamoto ya udondokaji wa wanafunzi na kuimarisha mazingira ya elimu jumuishi nchini.

Akizungumza Novemba 04, 2026 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa elimu maalumu na elimu jumuishi, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amewataka wadau kujadili kwa kina maandalizi ya kupokea makundi mawili ya wanafunzi kwa wakati mmoja (Double Cohort) mwaka 2028, kubaini sababu za udondokaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeachwa nyuma.

Mhe. Ameir amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika sekta ya elimu, hususan kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu. Amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, pamoja na mitaala, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau katika kuboresha miundombinu, upatikanaji wa vifaa na teknolojia saidizi pamoja na kuongeza uwezo wa walimu na wataalamu wanaohudumia wanafunzi hao.



Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Omar Hussein, amesema elimu ni haki ya msingi kwa kila binadamu bila kujali jinsia, hali ya ulemavu au changamoto nyingine, hivyo ni muhimu kwa wadau wote kushirikiana kuondoa vikwazo vinavyowazuia watoto wenye mahitaji maalumu kupata elimu bora, kukuza vipaji vyao na kutimiza ndoto zao.



Naye Afisa Elimu na Mratibu wa Ujumuishaji wa Watu Wenye Ulemavu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Tanzania, Sonia Pereira, ameipongeza Serikali kwa juhudi za kuimarisha elimu jumuishi na kueleza kuwa UNICEF inatarajia kushirikiana na Serikali kutekeleza programu inayofadhiliwa na ATscale, itakayowezesha watoto 2,000 kupata huduma za matibabu ya macho, sambamba na kuimarisha mfumo wa rufaa na huduma za afya ya macho nchini.



Awali, Mkurugenzi wa Elimu Maalumu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Margreth Matonya, amesema Serikali inaendelea kutekeleza programu mbalimbali za elimu jumuishi, zikiwemo zinazowawezesha watoto kusoma wakiwa nyumbani na wale wanaokaa hospitalini kwa muda mrefu, huku kikao hicho kikilenga kutathmini utekelezaji wa mkakati uliopita, kujadili Mkakati mpya wa Taifa wa Elimu Jumuishi na utekelezaji wa miongozo tisa ya elimu ili kuhakikisha kila taasisi inatekeleza wajibu wake katika kuimarisha elimu kwa wote.

No comments:

Post a Comment