Serikali imesisitiza umuhimu wa matumizi ya takwimu sahihi na zenye ubora katika kusimamia uchumi wa Taifa, kwa kuwa taarifa hizo ni msingi wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu mipango ya maendeleo, matumizi ya fedha za umma na uwekezaji katika sekta mbalimbali.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Mahafali ya 12 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Mhe. Munde alisema takwimu zina mchango mkubwa katika kuhakikisha rasilimali za Taifa zinatumika kwa ufanisi na kuelekezwa kwenye maeneo yenye mahitaji na matokeo makubwa kwa wananchi.
“Takwimu bora, zinatupa uwezo wa kutathmini kama matumizi ya fedha yanaleta matokeo yaliyokusudiwa na kama huduma zinawafikia wananchi”, alibainisha Mhe. Munde.
Alisema kuwa katika usimamizi wa uchumi na fedha za umma, maamuzi yanapaswa kuongozwa na ushahidi unaotokana na takwimu, badala ya kutegemea makadirio yasiyo na msingi wa taarifa sahihi.
Mhe. Munde alisisitiza kuwa matumizi ya takwimu ni muhimu katika kufanikisha Dira 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani, kuimarisha uwezo wa watu na maendeleo ya jamii, pamoja na kuhifadhi mazingira na kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
Alisema ili kufikia malengo hayo, Taifa linahitaji wataalamu wenye uwezo wa kuzalisha, kuchambua na kutumia takwimu katika kutambua fursa za kiuchumi, kuongeza tija na kupima matokeo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aliwaagiza wahitimu na wataalamu wote wa takwimu nchini kulinda usahihi wa taarifa, kuzingatia usiri na kuwasilisha matokeo ya uchambuzi kwa uaminifu.
Mhe. Munde alibainisha kuwa mapinduzi ya teknolojia na mabadiliko ya kidijitali yanaongeza umuhimu wa taaluma ya takwimu katika kuendesha biashara, kuboresha uzalishaji na kuongeza ufanisi wa huduma za umma.
“Ninawahimiza kutumia elimu yenu si katika kutafuta ajira tu bali pia kuanzisha shughuli za kiuchumi. Fursa zipo katika kilimo, utalii, viwanda, ujenzi na mali isiyohamishika, madini, uchumi wa buluu, michezo na ubunifu, huduma za kifedha na huduma nyingine”, alisema Mhe. Munde.
Alizitaja sekta za kilimo, utalii, viwanda, ujenzi, madini, uchumi wa buluu, huduma za kifedha na ubunifu kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa za kiuchumi ambazo wahitimu wanaweza kuzitumia kwa kutumia maarifa ya takwimu katika kutambua masoko, kupima mahitaji ya wateja na kufanya maamuzi bora ya uwekezaji.
Aidha, alitoa wito kwa wadau wa takwimu rasmi kushirikiana na Serikali katika kuandaa na kufuatilia viashiria vya maendeleo, hususan utekelezaji wa Dira 2050 na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.
Alisema takwimu hizo zitasaidia kupima mafanikio yaliyofikiwa, kubaini changamoto na kutambua makundi ambayo bado hayajanufaika ipasavyo na fursa za maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), Dkt. Tumaini Katunzi, alisema Chuo hicho kimepiga hatua kubwa kwa kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 439 mwaka wa masomo 2021/2022 hadi 2,152 mwaka 2025/2026, hatua inayoonesha kuongezeka kwa mahitaji ya wataalamu wa takwimu.
Alisema idadi ya wahadhiri wenye Shahada za Uzamivu pia imeongezeka kutoka watano hadi 16 katika kipindi hicho, huku programu za masomo katika ngazi mbalimbali zikiongezwa ili kupanua wigo wa uzalishaji wa wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika sekta za uchumi na maendeleo.
Dkt. Katunzi alisema katika kuimarisha nafasi yake kikanda, Chuo kimepanua ushirikiano na taasisi za ndani na nje ya nchi, ikiwemo Chuo Kikuu cha Torino cha Italia, Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia pamoja na Chuo Kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga cha Sayansi na Teknolojia nchini Kenya.
Alisema kupitia ushirikiano huo, chuo kimekuwa kikitoa mafunzo ya takwimu na uongozi kwa wataalamu wa nchi mbalimbali za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), hatua inayochochea ubadilishanaji wa maarifa na kuimarisha uwezo wa nchi wanachama kutumia takwimu katika kupanga na kusimamia maendeleo ya kiuchumi.
Picha za matukio mbalimbali katika Mahafali ya 12 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)











No comments:
Post a Comment