SHILINGI BILIONI 4.2 ZASOGEZA HUDUMA ZA MAHAKAMA KARIBU NA WANANCHI LUSHOTO – PROF. SHEMDOE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, November 22, 2026

SHILINGI BILIONI 4.2 ZASOGEZA HUDUMA ZA MAHAKAMA KARIBU NA WANANCHI LUSHOTO – PROF. SHEMDOE


Na: OWM–TAMISEMI, Lushoto


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, amepeleka Lushoto Shilingi Bilioni 4.2 kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya inayojengwa katika kata ya Magamba, hatua itakayowezesha wananchi kupata huduma za kimahakama kwa urahisi zaidi.

Prof. Shemdoe ameyasema hayo Novemba 21, 2026, alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhimiza uwajibikaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto.

“Kwenye Kata hii ya Magamba, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ametuletea Shilingi Bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hili la mahakama. Ni jengo la kisasa ambalo linaweza kuendesha hata kesi za kimataifa,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Ilani yake ya Uchaguzi, kiliahidi kuwajengea wananchi wa Lushoto mahakama, madarasa, barabara pamoja na kuwaletea huduma ya maji, na kwamba katika kata ya Magamba, ndani ya mwaka mmoja, tayari kimetekeleza zaidi ya asilimia 50 ya ahadi hizo, huku akisisitiza kuwa ahadi zote zilizotolewa kwa wananchi zitatekelezwa.

Aidha, Prof. Shemdoe amempongeza mkandarasi NAMIS kwa kutoa ajira kwa vijana na akina mama wa eneo hilo na kufikia asilimia 35 ya utekelezaji wa ujenzi wa mahakama hiyo licha ya changamoto za kijiografia zinazokabili eneo la mradi. Hata hivyo, amemtaka kuongeza kasi na ufanisi wa kazi ili jengo hilo likamilike kwa wakati na kuanza kuwahudumia wananchi wa Lushoto.

Naye, Diwani wa kata ya Magamba, Mhe. Stella Richard Kashamba, amesema mradi huo uliofikia asilimia 35 ya utekelezaji umeleta tabasamu kwa wananchi wa kata hiyo kutokana na vijana na akina mama kupata ajira na kujiongezea kipato. Amemshukuru Prof. Shemdoe kwa maelekezo aliyoyatoa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, yaliyomtaka mkandarasi kutoa ajira kwa wakazi wa eneo ambalo mahakama hiyo inajengwa.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi huo, Mhandisi Machimo Paul, amesema kazi zinazoendelea ni ujenzi wa kuta za matofali katika ghorofa ya juu baada ya kukamilika kwa sakafu ya ghorofa ya chini, na kwamba hatua inayofuata baada ya kukamilika kwa ujenzi huo ni kazi ya kuezeka jengo.

No comments:

Post a Comment