TAKUKURU YAZINDUA JENGO JIPYA LA OFISI KARATU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, November 1, 2026

TAKUKURU YAZINDUA JENGO JIPYA LA OFISI KARATU


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imezindua jengo jipya la ofisi wilayani Karatu, mkoani Arusha, lililojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 405.9 kwa lengo la kuimarisha mazingira ya kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Jengo hilo limezinduliwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin F. Chalamila, ambaye amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha uwezo wa taasisi hiyo katika kutekeleza majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini.


Chalamila amesema mradi huo umekamilika kwa gharama ya shilingi milioni 405.9, kiasi ambacho ni pungufu kwa shilingi milioni 15.5 ikilinganishwa na bajeti iliyokuwa imetengwa,akisisitiza kuwa matokeo hayo yanaonesha umuhimu wa usimamizi mzuri wa miradi na matumizi yenye tija ya fedha za umma.

Amepongeza wasimamizi wa ujenzi huo kwa kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, nidhamu ya matumizi ya fedha na muda uliopangwa, akieleza kuwa rasilimali za umma zinapaswa kutumika kwa uangalifu ili kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, amesema upatikanaji wa jengo hilo ni hatua muhimu katika kuboresha miundombinu ya taasisi hiyo mkoani humo, ambako kati ya wilaya sita, ni wilaya nne pekee zilizo na majengo ya ofisi zao, huku nyingine zikiendelea kutumia majengo ya kupanga.

Amesema kuwa na ofisi inayomilikiwa na taasisi kutasaidia kuboresha mazingira ya watumishi kutekeleza majukumu yao, kuongeza ufanisi na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuzuia na kupambana na rushwa.

Ngailo ameahidi kutumia fursa ya kuwa na ofisi hiyo kuboresha utoaji wa elimu kwa umma na kuimarisha mawasiliano na wananchi, ili kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Karatu,Lameck Karanga amesema uwepo wa jengo hilo utasaidia kuimarisha utendaji wa TAKUKURU na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, hususan katika masuala yanayohusu utoaji wa taarifa na ushirikiano na taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya rushwa.

Mbunge wa Jimbo la Karatu, Daniel Awaki, ameipongeza Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo, akieleza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya taasisi za umma ni muhimu katika kuongeza ufanisi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Karatu amepongeza hatua hiyo na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria na vitendo vya rushwa, akisisitiza kuwa ushiriki wa jamii ni muhimu katika kujenga uwajibikaji na kulinda rasilimali za umma.

Uzinduzi wa jengo hilo unatarajiwa kuwa chachu ya kuboresha mazingira ya utendaji wa TAKUKURU wilayani Karatu, kuimarisha ukaribu kati ya taasisi hiyo na wananchi pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa jukumu la kupambana na rushwa.

No comments:

Post a Comment