TANZANIA NA BENKI YA EXIM YA UTURUKI WAJADILI UFADHILI WA RELI YA SGR NA UKUAJI WA BIASHARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 12, 2026

TANZANIA NA BENKI YA EXIM YA UTURUKI WAJADILI UFADHILI WA RELI YA SGR NA UKUAJI WA BIASHARA

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Uturuki, Bw. Ali Guney baada ya kufanya kikao kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Reli ya SGR, kando ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi COP31, Jijini Antalya nchini Uturuki.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa nne kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Uturuki, Bw. Ali Guney (wa nne kutoka kulia) pamoja na ujumbe wa pande mbili (Tanzania na Exim Bank ya Uturuki), baada ya kufanya kikao kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Reli ya SGR, kando ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi COP31, Jijini Antalya nchini Uturuki. Baadhi yao katika picha ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Asha Khamis Abdulla (wa tatu kushoto) na Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade (wa pili kushoto).


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF-Uturuki)


Na Benny Mwaipaja, Antalya-Uturuki


Serikali ya Tanzania iko katika hatua za mwisho za mazungumzo na Benki ya Exim ya Uturuki ili kupata ufadhili wa dola za Marekani milioni 280 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kipande cha tatu na cha nne cha mradi wa reli ya kisasa (SGR).

Mazungumzo hayo yamefanyika Jijini Antalya nchini Uturuki, kando ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi COP31, kati ya ujumbe wa Tanzania ukiogozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar na Ujumbe wa Benki ya Exim ya Uturuki ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bw. Ali Guney.

Mhe. Balozi Omar alisema kuwa ujenzi wa mradi huo wa kimkakati wa SGR kipande cha tatu na nne wenye urefu wa zaidi ya kilometa 700, una thamani ya dola za Marekani bilioni 1.6 ambapo kiasi cha dola bilioni 1.32 kimeshapatikana, na kiasi cha dola milioni 280 ndicho kinachosubiriwa ili kukamilisha bajeti hiyo.

“SGR Ni mradi mkubwa wa miundombinu unaochukua zaidi ya kilomita 2,000, unaolenga kuunganisha jiji la bandari la Dar es Salaam kwenye pwani ya mashariki na mikoa ya magharibi ya Mwanza na Kigoma hadi nchi jirani, ikiwemo Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo” alisema Mhe. Balozi Omar

Alisema kuwa Mradi huo umegawanywa katika sehemu sita tofauti, zinazojulikana kama loti ambapo loti mbili za kwanza, zinazounganisha Dar es Salaam na Mji Mkuu wa Serikali, Dodoma, tayari zimekamilika na zinafanya kazi na kupokelewa vizuri na umma.

Mhe. Balozi Omar aliongeza kuwa, tofauti na miradi mingi ya reli ya kikanda inayotegemea dizeli, reli ya Tanzania (SGR) inatumia umeme, hatua inayoendana na ajenda ya Mkutano wa COP 31 unaofanyika Antalya-Uturuki, unaohimiza matumizi ya nishati safi ili kutunza mazingira na kuufanya mradi huo kuwa kielelezo endelevu cha usafiri wa kikanda.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Uturuki, Bw. Ali Guney, amesema kuwa Benki yake inathamini ujenzi wa mradi huo kwa maendeleo ya Tanzania na nchi jirani na kwamba Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo itakutana mwezi huu kujadili maombi ya ufadhili huo unaohitajika ili kukamilisha ujenzi wa Reli hiyo ya kisasa.

Bw. Guney alisema kuwa licha ya ujenzi wa Reli, Benki yake inaangalia pia maeneo mengine ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki katika nyanja za kiuchumi na kibiashra, ufadhili wa miradi ya miundombinu ya baadaye, ikiwemo barabara na madaraja, kama sehemu ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi.

Hatua hiyo inaendana na malengo ya biashara kati ya nchi mbili yaliyowekwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mhe. Recep Tayyip Erdogan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki ambao wamelenga ukuaji wa biashara kati ya Mataifa hayo mwili ufikie angalau dola za Marekani bilioni moja.

No comments:

Post a Comment