TANZANIA YAHITAJI SHILINGI TRILIONI 31.8 KUZIBA NAKISI YA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, November 14, 2026

TANZANIA YAHITAJI SHILINGI TRILIONI 31.8 KUZIBA NAKISI YA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, wakati wa Siku ya Fedha na Biashara uliofanyika kando ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi COP31, uliofanyika katika Banda la Tanzania, jijini Antalya ncini Uturuki
Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na wanajopo (Panelists), pamoja na baadhi ya Viongozi akiwemo Balozi wa Tanzania-Umoja wa Mataifa-Mhe. Balozi Togolani Mavura, kuliawakati wa Siku ya Fedha na Biashara, uliofanyika kando ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi COP31, uliofanyika katika Banda la Tanzania, jijini Antalya ncini Uturuki.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF, Antalya-Uturuki)

Na Benny Mwaipaja, Antalya, Uturuki


Tanzania, kwa kushirikiana na taasisi za fedha za kimataifa na washirika wa maendeleo, imetangaza hatua zitakazochukuliwa kukabiliana na nakisi ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 12 kati ya dola bilioni 19.3 zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi hususan katika Mpango wa Pili wa Taifa katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC2.0), hadi ifikapo mwaka 2030.

Hayo yameelezwa na Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, wakati Mkutano wa Pembezoni kwenye Siku ya Fedha na Biashara katika Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi COP31, uliofanyika katika Banda la Tanzania, jijini Antalya ncini Uturuki.

Amesema kuwa hatua hizo zinatokana na maazimio yaliyofikiwa wakati wa Majadiliano Kuhusu Upatikanaji wa Fedha za Ufadhili wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi wa Mwaka 2026 (Tanzania Climate Finance Roundtable)uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 5 Oktoba 2026.

Mpaka sasa Tanzania imefanikiwa kukusanya dola za Marekani bilioni 7.3, sawa na takribani shilingi za Tanzania trilioni 19.3 na kuhitaji kiasi kingine cha dola za Marekani bilioni 12, sawa na shilingi za Tanzania trilioni 31.8 zitakazotumika kuimarisha mfumo wa ufadhili wa mabadiliko ya tabia nchi, kuandaa miradi ya kipaumbele kwa uwekezaji na kukusanya fedha za umma na sekta binafsi. 

Amesema kuwa Mpango huo unaendana na Dira 2050, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31), Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi (2025–2035) na Mkataba wa Paris (Paris Agreement). 

Aidha, amesema kuwa mpango huo unajengwa juu ya mageuzi yanayoungwa mkono na ikiwemo Program ya Ustahimilivu na Uendelevu (Resilience and Sustainability Facility) chini ya Ufadhili cha Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Programu ya kujengea Ustahimilivu katika jamii ( Scaling-Up Locally Led Climate Action ) chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia na Programu ya Ustahimilivu wa Jamii dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi katika Ngazi za Mitaa (LoCAL- UNCDF) .

Bw. Bade amezitaja mbinu za nguzo tatu zitakazotumiwa na Serikali na washirika wake wa kimkakati kufikia lengo la kukusanya fedha hizo kuwa ni pamoja na kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Ufadhili wa Mabadiliko ya Tabia Nchi na kuimarisha taasisi zinazokusanya, kuratibu, kusimamia na kufuatilia fedha za mabadiliko ya tabia nchi.

“Mbinu hiyo itakuwa kuangalia uwezo wa kitaasisi, upangaji wa ufadhili wa tabia nchi, uwekaji alama kwenye bajeti (budget tagging), ufuatiliaji wa matumizi, mifumo ya fedha endelevu na ufuatiliaji kupitia mifumo iliyopo katika Wizara ya Fedha, Ofisi ya Makamu wa Rais, mamlaka za Zanzibar, wizara za sekta, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi za sekta ya fedha” alisema Bw. Bade.

Ameitaja nguzo ya pili kuwa ni kuandaa miradi ya kipaumbele cha kitaifa iliyo tayari kwa uwekezaji na yenye uwezo wa kuvutia wawekezaji (bankable projects). Huku Sekta za kipaumbele zikiwa kilimo kinachostahimili tabia nchi, usalama wa maji, nishati mbadala, kuokoa kuni kwa kupikia (clean cooking), miundombinu inayostahimili, usimamizi endelevu wa rasilimali asilia na uchumi wa bahari (buluu).

Amelitaja jambo la tatu kuwa ni upatikanaji wa mitaji kwa fedha endelevu na kupunguza vihatarishi kwa kutumia ufadhili mchanganyiko (blended finance), dhamana za mikopo (credit guarantees), bima ya tabia nchi, hati fungani za kijani na nyingine zenye alama, ufadhili unaotegemea matokeo, mikopo ya muda mrefu na ufadhili wa kaboni. 

“Misaada na fedha za masharti nafuu zitatumika kwa umakini kuongeza uwezekano wa miradi, kupunguza hatari na kuvutia mitaji ya kibiashara, uwekezaji wa kukabiliana na tabia nchi na ustahimilivu wenye manufaa makubwa kwa umma lakini faida ndogo ya kibiashara unapewa kipaumbele maalum” alisisitiza Bw. Bade.

Amesema kuwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kupitia AFRITAC East limejitolea kutoa mafunzo kuhusu uwekaji alama kwenye bajeti ya tabia nchi inapohitajika. Benki ya Dunia itaimarisha uwezo wa kiutendaji wa Vitengo vya Ufadhili wa Tabia Nchi (Climate Finance Units) Tanzania Bara na Zanzibar kupitia mradi wa SCALE.

Bw. Bade amesema Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limejitolea kuunga mkono Workstream 1; Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Workstream 2 hasa Kituo cha Uandaaji wa Miradi (Project Preparation Facility) kwa msisitizo wa kukabiliana na tabia nchi; na Mfuko wa Kimataifa wa Mazingira (GEF) umeonyesha nia ya kushiriki katika nguzo zote tatu, kwa msisitizo wa ufadhili mchanganyiko chini ya GEF-9.


No comments:

Post a Comment