
Mwakilishi wa Tanzania katika Muungano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua
(International Solar Alliance – ISA), Bw. Emilian Nyanda kutoka Wizara ya Nishati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa ISA unaoendelea nchini India. Mkutano huo umefunguliwa leo na Waziri anayeshughulikia masuala
ya Nishati Jadidifu wa India, Shri Pralhad Joshi ambaye ndiye anayeongoza Mkutano Mkuu wa 9 wa ISA.
New Delhi, India
Tanzania imetumia Mkutano Mkuu wa Tisa wa Muungano wa Kimataifa wa
Nishati ya Jua (International Solar Alliance – ISA) unaofanyika nchini
India, kueleza maeneo yanayohitaji ushirikiano katika uendelezaji wa
nishati jua ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji wa umeme
na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza tarehe 03 Novemba 2026 katika Mkutano huo unaohusisha nchi wanachama na Washirika wa Maendeleo zaidi ya 125, Mwakilishi wa
Tanzania katika ISA, Bw.Emilian Nyanda kutoka Wizara ya Nishati
amesema Serikali imeweka mkazo katika kuendeleza nishati jadidifu,
hususan nishati ya jua, ili kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika,
kuchochea shughuli za kiuchumi na kukabiliana na athari za mabadiliko
ya tabianchi.
Ameeleza kuwa, kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme kutoka gigawati 4.6 za sasa hadi gigawati 8 ifikapo mwaka 2030 na gigawati 70 mwaka 2050,
huku nishati ya jua ikitarajiwa kuwa miongoni mwa vyanzo muhimu vya
kufanikisha malengo hayo.
Katika hatua nyingine amesema Tanzania inapiga hatua katika uzalishaji
wa umeme wa jua kupitia miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa Kishapu
mkoani Shinyanga wenye uwezo wa kuzalisha megawati 150, ambapo awamu ya kwanza ya megawati 50 imekamilika na awamu ya pili ya megawati 100 ipo katika hatua za utekelezaji.
Ameongeza kuwa,kwa sasa megawati 100 za umeme jua zinaingia katika
gridi ya Taifa huku Serikali ikilenga kuongeza megawati 1,000 za
umeme huo wa jua ifikapo mwaka 2035 kupitia uwekezaji wa sekta ya umma
na binafsi.
Amesema Wizara ya Nishati kwa kushirkiana na TANESCO imeendelea na
jitihada za kutambua na kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya uwekezaji
wa miradi ya nishati ya jua, kufanya tafiti za upembuzi yakinifu na
tathmini za athari kwa mazingira, hatua inayolenga kupunguza gharama
za awali za uwekezaji na kuvutia wawekezaji zaidi nchini.
Kuhusu usambazaji wa umeme jua, amesema, pamoja na kuongeza mchango
wake kwenye gridi ya taifa, Tanzania inaendelea kutumia teknolojia ya
nishati hiyo kufikisha huduma katika maeneo ambayo hayajafikiwa na
Gridi ya Taifa, ikiwemo visiwa vilivyopo katika maziwa makuu na Bahari
ya Hindi.
Nishati hiyo pia inatumika katika shughuli za uzalishaji mali zikiwemo
kilimo, umwagiliaji, usindikaji wa mazao, uvuvi, ufugaji na usambazaji
wa maji.
Bw. Nyanda amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na ISA ambao
umewezesha kuanzishwa kwa Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Teknolojia
ya Nishati ya Jua (Solar Technology Application Centre - STAR-C)
katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), kinachotoa mafunzo kwa wataalamu
wa ndani, huku Watanzania wengine wakinufaika na mafunzo ya kitaalamu
katika taasisi mbalimbali za kimataifa.
Amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa
ISA, sekta binafsi na washirika wa maendeleo katika kuvutia mitaji,
teknolojia na utaalamu ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya
nishati jadidifu na kufanikisha azma ya Serikali ya kujenga uchumi
imara na endelevu kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mkutano huo umefunguliwa leo na Waziri anayeshughulikia masuala ya
Nishati Jadidifu wa India, Shri Pralhad Joshi ambaye ndiye anayeongoza
Mkutano Mkuu wa 9 wa ISA.
Katika hotuba yake ya ufunguzi Bw. Joshi amesisitiza umuhimu wa
mataifa yote kushirikiana ili kufanya nishati ya jua ipatikane kwa bei
nafuu duniani kote, pia ametoa wito wa kuongeza uwekezaji kwenye
nishati safi, hasa katika nchi zinazoendelea, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza maendeleo endelevu.

No comments:
Post a Comment