TANZANIA YAWEKA MSISITIZO MATUMIZI YA GESI ASILIA NA MAKAA YA MAWE COP 31 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, November 22, 2026

TANZANIA YAWEKA MSISITIZO MATUMIZI YA GESI ASILIA NA MAKAA YA MAWE COP 31


Tanzania imesisitiza na kuweka msimamo wa matumizi ya rasilimali za gesi asilia na makaa ya mawe katika shughuli za kijamii na kiuchumi badala ya kutegemea nishati ya mafuta ikiwa ni hatua mbadala ya kukabiliana na ongezeko la gesi joto.

Msimamo huo umetolewa Novemba 21, 2026 na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi mara baada ya kumalizika kwa mkutano baina ya Rais wa Majadiliano ya COP 31, Chris Bowen na Muungano wa Nchi zinazoendelea zilizopo katika kundi la G77 na China.

Amesema baada ya mazungumzo ya wiki mbili ya mkutano wa COP31, Nchi wanachama bado zinatofautiana na hazijafikia mwafaka kuhusu namna ya kuzuia ongezeko la joto duniani kwani rasimu ya azimio ya mkutano wa COP 31 iliyoandaliwa haina wito wa kuachana na matumizi ya nishati ya mafuta.

Amesema msimamo wa Tanzania ni kuhakikisha rasilimali za gesi asilia na makaa ya mawe unapewa kipaumbele kwa kuwa matumizi yake yatapunguza gharama na kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji.

“Rasimu ya azimio haina kipengele kilichotaka kuharakishwa kwa hatua za kuachana na vyanzo vya nishati ya mafuta hivyo mashauriano yataendelea hadi itakapokuwa wazi kwamba Nchi wanachama zimefikia mwafaka wa pamoja” amesema Dkt. Muyungi.

Dkt. Muyungi amesema Nchi zinazozalisha nishati ya mafuta hazijaonesha utayari wa kurejesha suala hilo kwani ajenda hiyo pia ilitawala majadiliano ya mkutano wa COP 30 uliofanyika nchini Brazil ambao ulimalizika bila hatua hizo kutajwa katika azimio lake la mwisho.

Aidha Dkt. Muyungi ameeleza masuala mengine yaliyoajiri katika mkutano huo wa Muungano wa G77 na China na Rais wa majadiliano ya COP 31 ni pamoja na kuongeza kasi na wigo wa upatikanaji wa fedha, ruzuku na mikopo nafuu kwa nchi na jamii zilizo mstari wa mbele katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ametaja ajenda nyingine ni suala la biashara na mabadiliko ya tabianchi ambalo limekuwa ni changamoto kwa mataifa yanayoendelea kwani huwekewa vikwazo mbalimbali ikiwemo madai ya wingi wa kaboni katika biadha mbalimbali zinazozalishwa.

Mkutano wa COP 31 umeingia siku pili ya majadiliano nje ya muda halisi wa kumalizika kwake tarehe 20, Novemba, 2026 mjini Antalya, Uturuki, huku wajumbe kutoka karibu nchi 200 wakiwa bado hawajafikia mwafaka kuhusu hatua za kupunguza matumizi ya nishati ya mafuta, gesi na makaa ya mawe.

No comments:

Post a Comment