CHAMA cha Wanawake Wachimbaji Tanzania (TAWOMA) kimeweka mikakati mipya ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia shughuli za uchimbaji wa madini, ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa maeneo salama ya uchimbaji, vifaa vya kisasa na urasimishaji wa shughuli zao.
Mikakati hiyo imekuja baada ya mwenyekiti wa chama hicho, Semeni John Malale, kuchaguliwa tena kuongoza TAWOMA kwa kipindi kingine cha miaka mitano, akiahidi kuimarisha ustawi wa wanawake wachimbaji na kukifanya chama hicho kujitegemea kiuchumi.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Malale amesema chama kinatarajia kutumia fursa na uwezeshaji unaotolewa na Serikali, hususan upatikanaji wa vifaa vya uchimbaji na maeneo yaliyofanyiwa utafiti, kuboresha shughuli za wanawake wachimbaji na kuongeza kipato chao.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa sehemu muhimu ya uwezeshaji wa wanawake katika sekta ya madini, ikiwemo upatikanaji wa mtambo wa kuchoronga unaotumika katika shughuli za utafiti wa madini.
Ameongeza kuwa wanawake hao wamepata fursa ya kupata maeneo ya uchimbaji yaliyofanyiwa utafiti, jambo litakalowasaidia kufanya shughuli zao katika maeneo salama na yenye uhakika zaidi wa uwepo wa madini.
“Tunamshukuru Mungu kwa kumaliza uchaguzi na kuniamini tena kuongoza chama hiki kwa miaka mitano. Tunaamini sasa tunakwenda kubadilisha maisha ya wanawake wachimbaji kwa kutumia fursa tulizopata, ikiwemo vifaa na maeneo ya uchimbaji,” amesema Malale.
Amesema katika kipindi chake kipya cha uongozi, TAWOMA inalenga kubuni miradi mbalimbali ya kiuchumi itakayokiwezesha chama kujitegemea badala ya kutegemea misaada, ruzuku na michango kutoka kwa wadau pekee.
Ametoa wito kwa wanawake wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini kujiunga na TAWOMA ili waweze kupata fursa za kujengewa uwezo, kushirikiana na kupata manufaa yanayotokana na sekta hiyo.
Pia ameiomba Serikali, hususan Rais Samia, kuendelea kuwashika mkono wanawake wachimbaji, huku akimpongeza Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kuendelea kusaidia upatikanaji wa vifaa vya uchimbaji.
Aidha, amempongeza Waziri wa Madini kwa juhudi za kuwezesha wanawake kupata maeneo ya uchimbaji kupitia mpango wa Mabadiliko ya Biashara Ndogo za Madini (MBT), akieleza kuwa maeneo yaliyotengwa yamefanyiwa utafiti ili kuongeza uwezekano wa wanawake kunufaika na shughuli za uchimbaji.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Msaidizi wa TAWOMA, Halima Mhando, amesema moja ya vipaumbele vyake katika nafasi hiyo ni kuimarisha mifumo ya chama ili kiweze kuwa na taarifa sahihi za wanachama, leseni zao na mahitaji yao.
Mhando amesema TAWOMA inapanga kuanzisha dawati maalumu la urasimishaji wa leseni litakalosaidia wanawake wachimbaji kupata elimu na msaada wa kufuata taratibu za kisheria katika shughuli zao.
Amesema dawati hilo litafanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Madini, Tume ya Madini, STAMICO pamoja na Ofisi za Wakuu wa Mikoa ili kuwafikia wanawake wengi zaidi, wakiwemo wale ambao bado hawajaingia katika mifumo rasmi ya uchimbaji.
“Tunataka kujenga mfumo utakaotuwezesha kujua idadi ya wanachama wetu, wenye leseni na wasio na leseni, wanaohitaji kuhuisha leseni na wale wanaohitaji msaada wa kurasimisha shughuli zao. Hii itatusaidia kupanga huduma kulingana na mahitaji halisi ya wanachama,” amesema Mhando.
Ameongeza kuwa chama pia kitaimarisha mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu ili kuwa na taarifa sahihi zitakazorahisisha mipango, ufuatiliaji na utoaji wa huduma kwa wanachama.
Mhando amesema lengo lingine ni kuwahamasisha wanawake ambao bado hawajajiunga na chama hicho kuingia katika mnyororo wa thamani wa madini, ili waweze kutumia sekta hiyo kama fursa ya kujiajiri na kujipatia kipato.
Amesisitiza kuwa TAWOMA inahitaji kuwa taasisi yenye mifumo imara ya kiutendaji na inayoweza kuwahudumia wanawake wachimbaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa ujumla, uongozi mpya wa TAWOMA unalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini, kuimarisha urasimishaji, kuongeza tija katika uchimbaji na kujenga chama chenye uwezo wa kujiendesha kiuchumi huku kikizingatia sheria, kulipa maduhuli na tozo za Serikali na kutekeleza wajibu wake kwa jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji.



No comments:
Post a Comment