TIRA YATAKIWA KUDUMISHA VIWANGO VYA KIMATAIFA VYA UBORA WA HUDUMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, November 18, 2026

TIRA YATAKIWA KUDUMISHA VIWANGO VYA KIMATAIFA VYA UBORA WA HUDUMA

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (Katikati), akipokea Cheti cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 iliyotolewa kwa TIRA, na Shirika la Ubora Tanzania -TBS, wakati wa hafla ya makabidhiano ya Vyeti vya Ubora iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo, Bima House, Njedengwa jijini Dodoma. Anayemkabidhi cheti hicho ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Ubora, wa Shirika la Ubora Tanzania -TBS, Mhandisi Abdallah Kileo (kulia), na kushoto ni Kamishna wa Bima nchini ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, akizungumza jambo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Cheti cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 iliyotolewa kwa TIRA, na Shirika la Ubora Tanzania -TBS, iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo, Bima House, Njedengwa jijini Dodoma, ambapo aliitaka Mamlaka hiyo kuhakikisha kuwa upatikanaji wa vyeti hivyo inakuwa chachu ya kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi na wadau wa sekta ya bima nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (kulia), akikabidhiwa Tuzo ya kutambua mchango wake katika Tasnia ya Bima, kutoka kwa Kamishna wa Bima nchini ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware, wakati wa hafla ya makabidhiano ya Cheti cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 iliyotolewa kwa TIRA, na Shirika la Ubora Tanzania -TBS, iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo, Bima House, Njedengwa jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (Katikati aliyeketi), Mkurugenzi wa Usimamizi wa Ubora, wa Shirika la Ubora Tanzania -TBS, Mhandisi Abdallah Kileo (wa pili kulia aliyeketi), na Kamishna wa Bima nchini ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware (wa pili kushoto aliyeketi), wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa TIRA, mara baada ya hafla ya makabidhiano ya Cheti cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 iliyotolewa kwa TIRA, na Shirika la Ubora Tanzania -TBS, iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo, Bima House, Njedengwa jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, akisalimiana na baadhi ya watumishi wa TIRA, wakati alipowasili katika mara baada ya hafla ya makabidhiano ya Cheti cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 iliyotolewa kwa TIRA, na Shirika la Ubora Tanzania -TBS, iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo, Bima House, Njedengwa jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma )


Na. Joseph Mahumi, WF, Dodoma


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, ameitaka Mamlaka hiyo kuhakikisha kuwa upatikanaji wa Cheti cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 unakuwa chachu ya kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi na wadau wa sekta ya bima nchini.

Ametoa msisitizo huo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Cheti cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 kwa TIRA, iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo, Bima House, Njedengwa jijini Dodoma, ambapo alisema kupata cheti hicho si mwisho wa safari ya ubora, bali ni mwanzo wa hatua nyingine ya kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo kwa kuzingatia viwango vinavyotambulika kimataifa.

Dkt. Mwamba alisema mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya TIRA katika kuimarisha mifumo yake ya kiutendaji, kuzingatia taratibu na viwango vya ubora, pamoja na kuongeza uwezo wa taasisi katika kutekeleza majukumu yake ya kusimamia na kuendeleza sekta ya bima nchini.

“Cheti hiki kisiwe pambo la ofisi au nyaraka ya kutunzwa kwenye mafaili pekee, bali kiwe kielelezo cha utamaduni wetu wa kazi na dhamira yetu ya kutoa huduma bora kila siku,” alisisitiza Dkt. Mwamba

Aidha alieleza kuwa Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (ISO 9001:2015) una umuhimu mkubwa katika kuimarisha michakato ya kazi, ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu, utatuzi wa changamoto na matumizi ya maoni ya wadau kama nyenzo ya kuboresha huduma zinazotolewa na taasisi.

Dkt. Mwamba alisema mafanikio ya TIRA katika kupata cheti hicho yanaendana na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza mageuzi ya kitaasisi na uimarishaji wa mifumo ya utoaji huduma ili kujenga taasisi imara, zenye ufanisi na zinazoweza kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa.

Akizungumzia mchango wa sekta ya bima katika uchumi wa Taifa, Dkt. Mwamba aliipongeza TIRA kwa juhudi za kusimamia sekta hiyo, kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma za bima na kuendeleza mazingira bora ya ukuaji wa soko la bima nchini ambapo mwaka 2025 ilichangia asilimia 2.11 ya Pato la Taifa.

“Natoa rai kwenu kuendelea kuzihimiza kampuni za bima nchini kuwekeza katika mifumo ya usimamizi wa ubora ili kuimarisha ushindani, kuongeza uaminifu wa wateja na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vinavyotambulika kimataifa” alisema Dkt Mwamba.

Alilipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa utaalamu, mwongozo na ushirikiano uliowezesha TIRA kufikia hatua hiyo, huku akilihimiza shirika hilo kuendelea kusaidia taasisi nyingine nchini kuimarisha mifumo yao ya usimamizi wa ubora.

Kwa upande wake Kamishna wa Bima nchini ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware, alisema kuwa Mamlaka hiyo inalenga kuhakikisha kuwa ofisi zake zote nchini zinafikia viwango hivyo ifikapo mwaka 2028.

Dkt. Saqware alisema kuwa katika kufikia azma hiyo, TIRA itaendelea kuimarisha maeneo mbalimbali ya utoaji huduma ikiwemo miundombinu na majengo ya ofisi, uwezo wa watumishi pamoja na michakato ya kiutendaji inayotumika katika kutoa huduma kwa wananchi na wadau wa sekta ya bima.

“TIRA itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na mifumo ya utoaji huduma ili kuhakikisha kuwa wadau wote, wakiwemo wananchi, Serikali, kampuni za bima, watumishi na watoa huduma, wanapata huduma zinazokidhi viwango vinavyotakiwa” alisema Dkt. Saqware.

Naye, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Ubora, wa Shirika la Ubora Tanzania -TBS, Mhandisi Abdallah Kileo, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TBS, alisema kuwa kupata Cheti cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 kwa TIRA ni hatua muhimu inayoonesha dhamira ya Mamlaka hiyo katika kuimarisha mifumo ya usimamizi, kuongeza ufanisi na kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi na wadau wa sekta ya bima zinakidhi viwango vinavyotambulika kimataifa.

Alisema kuwa uthibitisho huo unahusisha ofisi tano za TIRA, zikiwemo Makao Makuu ya Dodoma, Ofisi ya Zanzibar, Ofisi ya Dar es Salaam pamoja na Ofisi za Kanda ya Mashariki na maeneo mengine yaliyohusika katika utekelezaji wa mfumo huo.

“Mfumo huu wa ISO 9001:2015 unatoa mwongozo wa kuimarisha taratibu za usimamizi wa ubora, uwajibikaji na ufuatiliaji wa michakato ya kiutendaji, huku ukilenga kuhakikisha taasisi zinakidhi mahitaji ya wateja na kufanya maboresho endelevu ya huduma” alisema Mhandisi Kileo.

Aliongeza kuwa umuhimu wa mfumo huo kwa TIRA unatokana na ukubwa wa majukumu yake, yakiwemo kutoa leseni kwa kampuni na wadau wa sekta ya bima, kusimamia ushindani wa haki, kulinda maslahi ya wateja, kudhibiti shughuli za bima na kusimamia biashara za bima zinazovuka mipaka ya nchi, ambazo zinahitaji mifumo madhubuti ya usimamizi na uzingatiaji wa viwango vya ndani na kimataifa.

Alieleza kuwa TBS itaendelea kutoa huduma za upimaji, uthibitishaji na tathmini ya mifumo ya usimamizi wa ubora kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ubora, ufanisi na ushindani wa huduma na bidhaa nchini.

No comments:

Post a Comment