WANANCHI MOROGORO KUPATA HUDUMA ZA UPIMAJI WA MOYO NA MAGONJWA MENGINE BURE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 3, 2026

WANANCHI MOROGORO KUPATA HUDUMA ZA UPIMAJI WA MOYO NA MAGONJWA MENGINE BURE



NA SHUA NDEREKA, OKULY BLOG, MOROGORO


Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale, imeandaa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo na maradhi mengine bila malipo kwa wananchi wa jimbo hilo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wananchi kufahamu hali za afya zao na kuchukua hatua za mapema dhidi ya magonjwa.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya zoezi hilo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ally Mussa, alisema huduma hizo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, pamoja na kupunguza changamoto zinazowakabili katika upatikanaji wa huduma za matibabu.

“Matibabu haya, yatotolewa katika jimbo la kusini mashariki ambapo kiwango kikubwa Mhe. Mbunge ndiye mdhamana kwa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu, hivyo wananchi wajitokeze kwa wigi ili kupima afya zao” amesema Dkt Mussa.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo kupima afya zao na kupata ushauri wa kitaalamu utakaowawezesha kuchukua hatua stahiki mapema pindi wanapobainika kuwa na changamoto za kiafya.

Naye, Mbunge wa Jimbo hilo, Hamis Taletale, amesema amegaramia huduma hizo kwa lengo la kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi, akizingatia kuwa upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo huhusisha gharama kubwa ambazo zinaweza kuwa changamoto kwa baadhi ya wananchi.

Kwa upande wake, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Tulizo Shemu, amesema huduma hizo zitatolewa katika maeneo matatu ya tarafa ya Mikese, Ngerengere na Mkuyuni.

Amesema kuwa, zoezi hilo litatoa fursa kwa wananchi kufahamu hali za afya zao, kubaini changamoto zinazoweza kuwepo na kupata ushauri wa kitaalamu ili kuchukua hatua za mapema, jambo litakalosaidia kupunguza gharama zinazoweza kujitokeza endapo magonjwa yatagundulika katika hatua za baadaye.

“Uchunguzi huu utasaidia kubaini mapema, magonjwa ya moyo na viatarishi vyake ili kuweza kuwatibu watu mapema kabla ya kuingia katika madhara makubwa ya ugonjwa wa moyo” amesema Dkt. Shemu.

Kambi hiyo ya huduma za afya inatarajiwa kuanza Novemba 10 hadi Novemba 20, 2026, ambapo mbali na huduma za upimaji na matibabu, wataalamu wa lishe kwa kushirikiana na wahudumu wengine wa afya watatoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na kukabiliana na magonjwa ya moyo pamoja na maradhi mengine.


No comments:

Post a Comment