
Na: OWM – TAMISEMI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka maafisa bajeti wa halmashauri zote nchini kuhakikisha mipango ya bajeti inazingatia mahitaji ya mafuta kwa magari ya kubebea wagonjwa mahututi (ambulance), ili kuhakikisha yanakuwa tayari wakati wote kutoa huduma za dharura kwa wananchi.
Dkt. Nchemba ametoa agizo hilo leo, Novemba 9, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Iselamagazi, Shinyanga Vijijini, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, mkoani Shinyanga.
Amesisitiza kuwa upatikanaji wa ambulance pekee hautoshi bila kuhakikisha magari hayo yanakuwa na mafuta ya kutosha na yako katika hali nzuri ya kufanya kazi wakati wote ili kutoa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji msaada wa dharura.
Amesema hatua hiyo inalenga kumaliza changamoto ya wagonjwa kulazimishwa kuchangia gharama za mafuta ya magari hayo, jambo linalokwenda kinyume na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha ambulance zinakuwa msaada wa kuokoa maisha ya Watanzania kwa kutoa huduma za dharura kwa wakati.

Awali akizungumza katika mkutano huo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, anayeshughulikia masuala ya Afya, Dkt. Jafar Seif, amesisitiza ushirikiano kati ya viongozi wa halmashauri, wataalamu wa afya na viongozi wa maeneo husika katika kusimamia upatikanaji na matumizi ya ambulance hizo, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za usafiri wa dharura kwa wakati na kuboresha utoaji wa huduma za afya katika maeneo yao.

No comments:
Post a Comment