ZUNGU: UBUNIFU WA VIJANA USIISHIE KWENYE MAONESHO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 5, 2026

ZUNGU: UBUNIFU WA VIJANA USIISHIE KWENYE MAONESHO


Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, amezitaka taasisi za Serikali na sekta binafsi kutoa oda za bidhaa na teknolojia zinazobuniwa na vijana wa Kitanzania ili kuwasaidia kupata masoko na kukuza biashara zao badala ya kubaki na bunifu hizo kwenye maonesho.

Zungu ametoa wito huo Novemba 4,2026 jijini Dodoma baada ya kutembelea na kujionea bunifu mbalimbali zilizofanywa na vijana chini ya usimamizi wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akieleza kufurahishwa na kiwango cha teknolojia walichokionesha vijana hao.

Amesema miongoni mwa bunifu alizoziona ni vifaa vinavyoweza kusaidia kufuatilia vipimo vya afya ya mtu akiwa mbali na hospitali, teknolojia zinazolenga kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua pamoja na mitambo ya kudhibiti wadudu wanaoharibu mazao na kutenganisha maji na gesi.

Kwa mujibu wa Zungu amesema bunifu hizo zinaonesha uwezo mkubwa wa vijana katika kutumia sayansi na teknolojia kutatua changamoto zinazokabili jamii, hivyo zinahitaji kuungwa mkono ili ziweze kufikia hatua ya uzalishaji na matumizi katika soko.

Katika hatua nyingine, Zungu ameibua hoja kuhusu matumizi ya shilingi bilioni 200 zilizotengwa kwa ajili ya kuwawezesha vijana, akitaka kufahamu kama fedha hizo ziliwafikia walengwa na kama hazikuwafikia, zilielekezwa kwa nani na kutumika katika shughuli zipi.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameeleza kuwa uwekezaji katika elimu ya sayansi, tafiti na kuwawezesha wabunifu kuingiza bidhaa sokoni ni miongoni mwa hatua zinazolenga kukuza uwezo wa vijana wa Kitanzania.

Amesema pamoja na Tanzania kuwa na kazi kubwa ya kufanya ili kufikia maendeleo zaidi ya sayansi na teknolojia, uwezo unaooneshwa na vijana unatoa matumaini ya mafanikio katika siku zijazo.

"Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika eneo hilo kupitia ufadhili wa masomo ya sayansi kwa wanafunzi hususani wasichana, utoaji wa tuzo kwa wahadhiri waliofanya tafiti zinazotambulika kimataifa pamoja na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi,"amesema. 

No comments:

Post a Comment